1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kijasusi za Urusi kuongezeka nchini Ujerumani

22 Juni 2023

Shirika la ujasusi wa ndani la Ujerumani limeonya kuwa operesheni za kijasusi za Urusi zinatarajiwa kuongezeka nchini humo na vuguvugu la mrengo mkali wa kulia linatumia upinzani dhidi ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Symbolbild IT-Systeme
Picha: Jochen Tack/IMAGO

Ofisi ya Shirikisho ya Ulinzi wa Katiba ya Ujerumani (BfV) pamoja na shirika la ujasusi wa ndani la nchi hiyo, zimesema kuwa shughuli za kijasusi za Urusi na habari za upotoshaji viliongezeka mno mnamo mwaka 2022 nchini Ujerumani na wanakadiria kuwa hali hiyo itaendelea pia mwaka huu.

Katika ripoti mpya iliyochapishwa Jumanne, BfV imesema Urusi imekuwa ikionyesha nia ya kuzidisha kampeni za upotoshaji. China pia ilitajwa kuwa mmoja wa "wahusika wakuu" katika operesheni za kijasusi nchini Ujerumani.

Ripoti hiyo inabaini kuwa katika siku zijazo, kunaweza kutarajiwa operesheni zaidi na za siri za kijasusi pamoja na mashambulizi ya kimtandao kutoka kwa Urusi, na kuongeza kuwa mashambulizi hayo ya  kimtandao mara nyingi hulenga kupata taarifa, lakini pia yanaweza kuwa ya hujuma au kutumikia madhumuni husika kwa aina fulani ya ushawishi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser ameandika katika dibaji ya ripoti hiyo kuwa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vinamaanisha pia mabadiliko katika sera za usalama wa ndani, hasa wakati huu wa vita ambapo uongozi wa Ikulu ya Urusi ya Kremlin unategemea mno ripoti zake za kijasusi.

Rais waBfV Thomas Haldenwang ameongeza kuwa ripoti ya BfV  kwa mara nyingine tena inaangazia hatari kwa usalama wa ndani wa Ujerumani kutokana na vitendo vya ujasusi, harakati za mtandaoni na majaribio ya idara za kijasusi za kigeni kujaribu kuwa na ushawishi, vitendo ambavyo vimekuwa vya kisasa zaidi na vigumu kuzuilika.

Soma pia: Jasusi wa Urusi akamatwa nchini Ujerumani

Harakati za China hata hivyo zinalenga hasa kukusanya taarifa kuhusu sekta ya viwanda ya Ujerumani, taasisi za kisayansi na kijeshi. Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa mnamo mwaka wa 2022, watu wanaoshukiwa kuwa wahusika wa serikali ya China waliendelea kufanya mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya wafanyabiashara, mashirika ya serikali na watu binafsi, na pia dhidi ya taasisi za kisiasa.

Kuficha misimamo mikali ya mrengo wa kulia

Viongozi wa BfV wakiwa katika mazungumzo mjini Berlin (17.10.2022)Picha: Nikita Jolkver/DW

Ripoti ya BfV pia imebaini kuongezeka kwa idadi ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani, na idadi hiyo sasa imefikia watu 38,800, (kutoka 33,900 mwaka 2021), huku kati yao 14,000 wakionekana kuwa na muelekeo wa vurugu.

Shirika hilo pia limebaini kuwa vuguvugu la mrengo wa kulia lilmebadili mfumo wao na sasa linadhihirisha misimamo yao hadharani. Mwanzoni mwa mwaka 2022, ripoti iligundua kuwa watu wa mrengo mkali wa kulia walikuwa wakichochea maandamano dhidi ya hatua za kupambana na UVIKO-19.

 Pia mwishoni mwa mwaka jana, watu wa mrengo wa kulia  walikuwa na matumaini ya kuamsha hisia za upinzani kwa kuhusisha kitendo cha Ujerumani kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine na mzozo wa nishati nchini humo. Mara tu baada ya azma hiyo kushindwa kupata uungaji mkono wa umma, BfV imesema, vuguvugu la mrengo wa kulia kwa mara nyingine tena lilikuwa na matumaini ya kuchochea hisia za umma kwa kupinga suala la wahamiaji.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW