1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kutunza mazingira katika mji wa Nairobi

29 Oktoba 2018

Kundi la Kombgreen linaendeleza harakati za kutunza mazingira katika mji wa Niarobi. vijana waliokuwa wahalifu sugu mtaani Korogocho wameamua kuwa mfano na kioo ya jamii kwa kutengeza bustani ukingoni mwa mto Nairobi.

ehemals gewalttätige Jugendliche beschäftigen sich mit der Wiederherstellung des Nairobi Flusses
Picha: DW/T. Mwadzaya

Vijana wa mtaa wa Korogocho waliokuwa wahalifu sugu na kuamua kuachana na kasumba hiyo wameanzisha harakati za kutunza mazingira katika mji wa Niarobi, ambapo kupitia kundi lao la Kombgreen wanaedesha mradi wa kutengeneza bustani kwenye kingo za mto Nairobi.

Mto wa Nairobi ulio na vijito kadhaa vidogo uko katika hali mbaya na harakati zinaendelea kuusafisha.Chanzo chake ni eneo la Mlima Kenya. Mamlaka ya mazingira nchini Kenya ya NEMA imekuwa ikibomoa majengo yaliyoko ukingoni mwa mito kama hatua ya kwanza ya kuligeuza jiji. Katika harakati kama hizi, vijana waliokuwa wahalifu sugu mtaani Korogocho wameamua kuwa mfano na kioo katika jamii kwa kuyasafisha mazingira na kutengeza bustani ukingoni mwa mto Nairobi.

Daraja la Korogocho ndiko unakopitia mto wa Nairobi ufikapo mtaani Dandora.Kwa lugha ya mtaani neno Korogocho lina maana ya msongamano ambao ni dhahiri kwani vijumba vya mabati na mbao ndio vingi kila unakotazama. Eneo la kulia lina nyasi na bustani la kijani kibichi linalovutia ndio mandhari unayokutana nayo kulikokuwa jaa la taka. Ijapokuwa  mto Nairobi sio nadhifu na maji yake sio salama, angalau mazingira yamebadilika. Sasa wakazi wanaweza kubarizi hali ya hewa ikiridhia.

Walinzi wa daraja la Korogocho

Daraja la Korogocho iliko bustani ya kipekee ukingoni mwa Mto NairobiPicha: DW/T. Mwadzaya

Nusu ya wakazi wa jiji la Nairobi wanaishi kwenye mitaa ya mabanda inayofanana kama vile Korogocho, Mukuru kwa Njenga, Mukuru Kayiaba, Mathare na Kibera. Ni jambo la kawaida kuwaona baadhi ya wakazi wakimimina taka kwenye mto wa Nairobi huko Korogocho bila hofu yoyote. Hii ni kwasababu hakuna mfumo maalum wa kuzoa na kutupa taka.Chanzo cha Mto wa Nairobi ni eneo la Mlima Kenya na ni sehemu ya Mto Sagana na Tana ambao ndio mrefu zaidi nchini Kenya.

Hata hivyo mto huo ukiwasili Korogocho hautamaniki.Hilo ndilo lililowasukuma vijana waliokuwa wahalifu mtaani humo kulisafisha eneo la ukingo wa mto na kuunda bustani la kubarizi. Mradi wao ulianza mwaka uliopita wa  2017 kwenye daraja la Korogocho.

"Hili daraja likijengwa sisi ndio tulikwa walinzi ili watu wasiibe hivyo vyuma.Daraja lillipokamilika tukaona bado tunawapoteza vijana wenzetu.Tukajiuliza kama vijana tufanyeje? Ndio tukaamua tuunde bustani dogo, ili vijana waweze kuja pamoja na kubadilishana mawazo na kuachana na wizi. Huu mradi umetusaidia sana hata wasichana wetu waliokuwa wanajiuza waliacha,” anasema Frederick Okinda, mwanachama wa kikundi cha Kombgreen kinachowaleta pamoja vijana waliokuwa wahalifu sugu mtaani Korogocho.

Chanzo cha kuacha uhalifu

Katika kipindi cha tangu mwaka 2010 hadi sasa vijana wasiopungua 20 waliuawa kwa kupigwa risasi walipopatikana wakiiba mtaani humo. Hilo liliwafanya kushika sikio na kuamua kuifuata njia ya sawa na kuuasi ukora. Hii ni mara ya nne kwa serikali ya Kenya kujitahidi kuusafisha mto wa Nairobi na jiji zima kwa jumla.

Mwaka 2009 marehemu waziri wa mazingira John Michuki alimiminiwa sifa kwa kuufufua Mto Nairobi uliochafuliwa na kinyesi na taka za viwanda.Tatizo bado lipo miaka kadhaa baada ya kifo chake. Awamu ya kwanza ya mradi wa kuusafisha mto huu ilianza mwaka 2007 kwa gharama ya shilingi bilioni 16.

Mwezi Aprili mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta aliamuru shughuli hiyo kufanyika ili kuunusuru mto wenyewe na jiji la Nairobi linalokabiliana na milima ya taka. "Hilo husababisha mafuriko na matatizo mengine yanayowapa dhiki wakazi wa Nairobi", alisema Rais Kenyatta na kuahidi kuwafikisha mbele ya sheria maafisa wa serikali waliotoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo yanayopakana na Mto Nirobi.


Sehemu ya Mto NairobiPicha: DW/T. Mwadzaya

Usafi wa kwanza wa Mto Nairobi

Hii ni mara ya nne kwa mradi wa kulisafisha jiji la Nairobi na mito yake kuzinduliwa tangu 1999. Mwaka 2001 na 2003 juhudi kama hizo zilipewa kipaumbele ila bila mafanikio. Hata hivyo vijana wa kikundi cha Kombgreen cha Korogocho wanaonekana kufanikiwa. Vijana hao waliokuwa wahalifu walisaka ushauri wa mwanamazingira na mwanaharakati Sam Dindi ambaye amekuwa akiwaelekeza kuhusu  njia mbadala za kuubadili sura ukingo wa Mto Nairobi.

Yeye amesomea mazingira na aliwahi kufanya tathmini ya mbinu mujarab za kufufua maeneo ya kingo za mto akiwa katika chuo kikuu cha Moi na anasema kuna sehemu moja ya mto ilikuwa jaa na waliweza kulibadili likawa bustani ndogo. Wakazoa takataka, wakapanda nyasi na kwa sasa ni sehemu ya mapumziko.

Kina mama wakitaka kusuka nywele wanakuja hapo na vijana wanakaa pale wakipiga soga. Askari nao wakitaka kuzungumza nao hawawaiti kwenye police station. Wanawafuata kwenye bustani hiyo yenye upana wa takirabani mita 200. "Mto wa Nairobi wote ukiweza kutengezwa kutakuwa na amani na ukora utapungua,” anasema Dindi.


Bustani iliyoko ukingoni mwa mto Nairobi eneo la KorogochoPicha: DW/T. Mwadzaya

Risasi na changamoto

Vijana hao wameacha uhalifu na kukumbatia juhudi za kuusafisha mto Nairobi kwenye eneo la Korogocho. Mto Nairobi unafuata njia ipitayo katikati ya jiji la Nairobi. Maji yote ya bonde la mto jijini Nairobi yanakusanyika eneo la mashariki na kukutana na Mto Athi kabla ya kuelekea kwenye bahari ya Hindi.

Mito ya jiji la Nairobi inatatizwa na taka za kinyesi na viwanda zinazotupwa kiholela.Katika msimu wa mvua hilo husababisha mafuriko na mto kuvunja kingo zake. Juhudi za vijana wa kikundi cha Komb Green cha Korogocho zina azma ya kulitafutia tatizo hilo suluhu.

Hata hivyo zipo changamoto kadhaa. Mzee Moses Muchina Muteru, mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 anasema maisha yake yote yamezongwa na uhalifu. Kwa sasa ameacha ukora na ni mmoja ya waelekezi wa vijana wa KombGreen.

”Tunana shida ya mashine ya kukata hizi nyasi.Tunateseka kwasabu zikikua tunaziacha tu zikanyagwe ndio zirejee chini ila zinatakiwa kukatwa baada ya wiki mbili. Pale darajani tuna tangi moja la maji tuliloachiwa na NYS.Tunatumia maji hayo kusafishia pikipiki na magari. Shida tuliyoko nayo ni mashini ambayo tunaomba kwa wafadhili,” anaweka bayana.

NEMA na uhifadhi wa kingo za mito

Wanachama wa Kikundi cha KombGreen tayari wamewasilisha pendekezo kwa gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko kutaka kushirikishwa na mipango ya kuufufua Mto Nairobi kwenye maeneo mengine kadhalika msaada  wa nyenzo.

Mipango hii ya kikundi cha Komb green cha Korogocho inaoana na ile ya mamlaka ya mazingira nchini Kenya, NEMA, inayosimamia mradi wa kuwashajiisha wakazi wa bonde la mito ya Nairobi kufufua na kuhifadhi eneo hilo. Mradi huo ulioko kwenye awamu ya majaribio utatumika kama muongozo kwa maeneo mengine ya nchi.

Dhamira ni kuwasogeza karibu wakazi na harakati za kuhifadhi mazingira ya kingo za mito. Hadi hapo msikilizaji hatuna cha ziadakwenye makala hii ya mazingira , tumeangazia juhudi za kulifufua na kuhifadhi eneo la kingo za mto Nairobi nchini Kenya.

Mwandishi: Thelma Mwadzya

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW