Harakati za kuwania kombe la mataifa ya bara Afrika - AFCON zaendelea
6 Januari 2012Botswana hii leo watajipima nguvu dhidi ya Zimbabwe, huku nyota wao, Jerome Ramatlhakwane, akiwa na kiu ya kufunga mabao mengi. Mchezaji huyo ndiye aliyekuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa the Zebras jinsi wanavyofahamika wanafuzu katika dimba hilo kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza mbele ya Tunisia, Malawi, Togo na Chad.
Nchini Mali kiungo wa Barcelona, Seydou Keita, amerejea tena katika kikosi cha taifa baada ya kutajwa katika orodha ya mwanzo ya wachezaji watakaoshiriki dimba la ubingwa wa Afrika. Naye mchezaji Nando Rafael, ambaye alitoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola akiwa mtoto, ametajwa katika kikosi cha taifa kitakachoshiri fainali hizo. Angola iko katika kundi B pamoja na Burkina Faso, Cote divoire, na Sudan.
Wikendi hii michuano ya duru ya tatu ya kombe la FA nchini Uingereza itasakatwa ambapo hii leo, jumamosi, Newcastle itakuwa na kibarua kikali dhidi ya Blackburn Rovers. Newcastle watakuwa bila ya huduma za mshambulizi wake matata, Demba Ba, na kiungo wa kati, Cheick Tiote, ambao wako nje kwa wiki kadhaa ili kuyawakilisha mataifa yao ya Senegal na Cote idivoire mtawalia katika mechi za mataifa bingwa barani Afrika, AFCON.
Katika mchuano mwingine wa leo jumamosi Tottenham Hotspurs itaikaribisha Cheltenham Town katika uga wa WhiteHart Lane.
Kesho Manchester City itawakaribisha Manchester United na unaonekana kuwa ni mchuano wa kulipiza kisasi. City waliwashangaza wengi mwezi Oktoba walipowarindima United magoli sita kwa moja uwanjani Old Trafford , matokeo ambayo mkufunzi Alex ferguson aliyataja kuwa siku mbaya zaidi katika taaluma yake ya soka. Tangu ushindi huo, City wamekuwa wakiongoza ligi ya Primia mbele ya United, na sasa wako alama tatu mbele. City watakuwa bila ya wachezaji Mario Balotelli na Gareth Barry, wote kutokana na majeraha, na ndugu wawili, Yaya Toure na Kolo Toure, ambao wameondoka kwa kibarua cha taifa nchini Cote dIvoire katika mechi za ubingwa wa Afrika.
Mchuano mwingine utakaosakatwa kesho, jumapili, ni kati ya Chelsea na Portsmouth uwanjani Stamford Bridge. Siku ya Jumatatu Arsenal watawakaribisha Leeds United ugani Emirates, mchuano ambao huenda ukamkaribisha tena Thiery Henry katika timu ya Arsenal. The Gunners walikamilisha mkataba wa mkopo utakaomwezesha Henry kuwachezea tena baada ya mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 34 wa klabu ya Marekani, New York Red Bulls, kukubali kurejea Emirates kwa mkataba wa mkopo wa miezi miwili. Mfaransa huyo aliichezea Arsenal mara 370 na kufunga mabao 226.
Hapa nchini Ujerumani, Mkufunzi wa Wolfsburg, Felix Magath, ameendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kumnyakua beki Mbrazil, Felipe Lopes, na kiungo wa kati wa Cote dIvoire, Ibrahim Sissoko, na kufikisha saba idadi ya wachezaji wapya aliowasajili tangu siku ya krismasi. Nayo klabu ya Borussia Moenchengladbach imemsajili kiungo wa kati Alexander Ring kutoka Finland kwa mkopo kutoka kwa mabingwa wa Finland HJK Helsinki.
Nao inter Milan wamethibitisha kuwa klabu hiyo imefanya mazungumzo na wawakilishi kutoka klabu ya Manchester City huku mchezaji Carlos Tevez akidhaniwa kuwa ajenda kuu. Hata hivyo, klabu hiyo ya Italia ilikanusha kuwa mazungumzo hayo yalikuwa kumhusu mchezaji kiungo Mholanzi , Wesley Sneijder. Mapema wiki hii kulikuwa na ripoti kuwa Inter walitaka kumnyakua Tevez anayedhaniwa kugharimu pauni milioni 25 na kuwapiku mahasimu wao wa mji wa Milan baada ya mazungumzo baina ya AC Milan na Man City kukwama.
mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Miraji Othman