Harakati za mkataba wa amani nchini Colombia
14 Oktoba 2016Uamuzi huo unajiri huku Santos na kundi lake wakipokea maoni kutoka kwa waakilishi wa wale waliopiga kura dhidi ya mkataba huo walioutaja kuwahurumia mno waasi hao wa kundi la FARC.
Baadaye atawasilisha mapendekezo hayo kwa viongozi wa kundi hilo la FARC huko Havana ambao wamesema wako tayari kuzungumzia mapendekezo mapya.
Santos alisema kuwa aliamua kuongeza muda huo wa kusitisha mapigano baada ya mkutano na viongozi wa wanafunzi waliokuwa wameandaa maandamano mawili makubwa katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo, Bogota kuonyesha uungwaji mkono kwa mkataba huo wa amani.
Santos alisema , "mwanafunzi mmoja alinikumbusha kuwa katika jeshi na vyeo vya kundi hilo la waasi, kuna vijana wanaosubiri kuona kitakachotokea na kutumaini kuwa haitawabidi kutumia tena bunduki." Alisema hayo katika hotuba yake kupitia runinga.
Matumaini ya amani
Muda wa kusitishwa kwa mapigano unaweza kuongezwa zaidi lakini Santos amesema kuwa anamatumaini kuwa mkataba utaafikiwa kabla ya muda huo kukamilika .
Lakini upande unaopinga mkataba huo unaoongozwa na aliyekuwa rais Alvaro Uribe , unataka waasi waliofanya uhalifu wa kivita kufungwa kwa muda wa kati ya miaka mitano hadi minane ikiwezekana katika mashamba ya kilimo na kuzuiwa kushikilia wadhifa wowote wa kuchaguliwa.
Kulikuwa na malalamishi kuwa mkataba huo ulipendekeza nafasi 10 za ubunge kwa kundi hilo la waasi na vifungo visivyokuwa vya kawaida kama vile kusafisha migodi badala ya vifungo vya magerezani ili kutamatishwa kwa mapigano hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu laki 2 na elfu 20.
Ijapokuwa uongozi wa kundi hilo la waasi la FARC wamesema wako tayari kupokea mapendekezo mapya, mapendekezo ya Uriba yatakuwa magumu kukubalika ikitiliwa maanani kwamba kundi hilo limekataa uwezekano wa kifungo cha jela na kutaka kuunda chama cha kisiasa.
Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yalioafikiwa mwezi Agosti yalifutiliwa mbali wakati mkataba huo wa amani ulipokataliwa mapema mwezi huu.
Santos alishinda tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu Ijumaa iliyopita kwa juhudi zake za kutamatisha vita.
Mwandishi: Tatu Karema/afpe,ape
Mahriri: Gakuba Daniel