HARARE: Mugabe atagombea tena uchaguzi wa rais
31 Machi 2007Nchini Zimbabwe,chama tawala ZANU-PF kimemteua Rais Robert Mugabe kugombea tena urais katika uchaguzi unaotazamiwa kufanywa mwakani.Uamuzi huo ulipitishwa na kamati kuu ya ZANU-PF kwenye mkutano uliofanywa katika mji mkuu Harare.Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha MDC,Tendai Biti amesema,uamuzi huo ni msiba kwa nchi hiyo.Chama hicho cha upinzani pia kimesema,Mugabe mwenye umri wa miaka 83 ameshaiongoza vibaya nchi hiyo kwa miaka 27.Wakati huo huo msemaji wa serikali ya Marekani mjini Washington amesema,uamuzi wa kumruhusu Mugabe kugombea tena awamu nyingine ni wa kusikitisha.Marekani pia imesikitishwa hasa na viongozi wa serikali na wa nchi zilizo jirani na Zimbabwe,ambao katika mkutano wao wa kilele hivi karibuni nchini Tanzania,walijiepusha kumkosoa Mugabe na badala yake wametoa wito wa kuondosha vikwazo viliyvowekwa na nchi za magharibi dhidi ya Zimbabwe.Rais Mugabe amezidi kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa baada ya polisi hivi karibuni,kutumia nguvu dhidi ya wapinzani wa kisiasa nchini Zimbabwe.