HARARE : Mugabe azishutumu Uingereza na Marekani kwa ubaguzi
19 Septemba 2005Kiongozi wa Zimbabwe ameushutumu Umoja wa Mataifa na Uingereza kwa ubaguzi wa rangi na undumila kuwili juu ya haki za binaadamu na kusema kwamba shirila la makaazi la Umoja wa Mataifa linapaswa kushirikiana na wahanga wa kimbunga wa Marekani na sio Wazimbabwe walioachwa bila ya makaazi kutokana na hatua za serikali kuvunja makaazi duni.
Rais Robert Mugabe amehoji kwa nini serikali yake imeshutumiwa kwa hatua yake hiyo iliyoacha watu 700,000 kukosa makaazi wakati Uingereza na shirika la Habitat lenye makao yake mjini Nairobi Kenya yamebakia kimya juu ya hatua iliyochokuliwa na Marekani kukabiliana na maafa ya kimbunga Katrina.
Amesema wamekaa kimya juu ya mazingira ya kufadhaisha ya kile kinachoonekana wazi ni dharau ya serikali kwa maafa ya Ghuba ya Mwambao nchini Marekani ambapo jamii nzima ya watu wengi wao wakiwa ni weusi imeachwa kwa makusudi kuatilika na madhara ya kimbunga hicho wakiwa kama kondoo wa kutolewa muhanga.
Rais Mugabe alikuwa akizungumza katika siku ya pili ya mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo jana.