HARARE : Polisi yazidi kukamata viongozi wa biashara
8 Julai 2007Serikali ya Zimbawe imewatia mbaroni viongozi 16 zaidi wa biashara kwa kupandisha bei za bidhaa juu ya zile zilizotangazwa na serikali ya Rais Robert Mugabe.
Kwa mujibu wa gazeti lka serikali la Sunday Mail kukamatwa kwa watendaji hao wakuu wa biashara kumefanya idadi ya viongozi waliokamatwa kufikia 33 tokea Ijumaa chini ya msako wa polisi uliopewa jina la Operesheni Punguza Bei.Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na wakurugenzi wa kampuni ya Edgars muuzaji mashuhuri wa nguo za reja reja na wamiliki wa maduka makubwa ya bidhaa na gesi.
Polisi imetishia kutanuwa msako wao kwenye soko la mitumba, maduka ya madawa,bidhaa za ujenzi na katika soko lisilo la sekta rasmi mjini Harare ambapo wakaazi wa jiji hupendelea kununuwa bidhaa za bei nafuu za nguo,viatu na elektoroniki.
Serikali ya Mugabe wiki mbili zilizopita iliwaonya wafanya biashara kwa kuwataka wapunguze bei za bidhaa kwa asilimia 50 venginevyo biashara zao zitataifishwa na serikali.