Harare. Tsvangirai atiwa korokoroni.
12 Machi 2007Mawakili nchini Zimbabwe wanaomtetea kiongozi mkuu wa chama cha upinzani wanadai kuwa Morgan Tsvangirai ameshambuliwa na kuteswa na polisi. Kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change alikamatwa pamoja na maafisa wengine wa vyama vya upinzani wakati wakiwa njiani kuhudhuria mkutano wa kuipinga serikali, ambao pia unaelezwa kuwa ni mkutano wa maombi , katika mji mkuu Harare.
Mmoja wa waandamanaji alipigwa risasi na polisi na kufa katika ghasia hizo na duru zinaeleza kuwa watu wengine wamekamatwa katika matukio yanayohusiana na hayo.
Msemaji wa polisi amesema kuwa Tsvangirai amekamatwa kumzuwia kuwashawishi watu kufanya matendo ya ghasia. Hali ya wasi wasi inazidi nchini Zimbabwe wakati ughali wa maisha unazidi kupanda na ukosefu wa nafasi za kazi ukifikia asilimia 80.