HARARE-Upigaji kura wanedelea nchini kote Zimbabwe.
31 Machi 2005Wananchi wa Zimbabwe wamo katika zoezi la upigaji kura kuchagua Bunge jipya.Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema leo asubuhi,ambapo Rais Robert Mugabe ameonesha matumaini makubwa,chama chake kinachotawala cha ZANU-PF,kitaibuka na ushindi utakaomuwezesha kujiimarisha zaidi katika madaraka ya kuingoza Zimbabwe.Chama cha Zanu-PF kinatawala Zimbabwe kwa miaka 25 mfululizo.
Watu milioni sita wenye uwezo wa kupiga kura,wanatazamiwa kujitokeza kupiga kura zao baada ya wiki kadhaa za kampeni,ambazo safari hii zilikuwa shwari bila umwagikaji wa damu,kulinganishwa na uchaguzi uliopita.Hata hivyo vikundi vya kutetea haki za binadamu,vimesema kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki,kwa maelezo kuwa maelfu ya watu waliokwishafariki dunia wameorodheshwa kupiga kura na pia kumekuwa na ripoti za watu kunyanyaswa,halikadhalika misaada ya chakula imezuiliwa kwa watu wanaounga mkono upinzani.
Chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change-MDC,kimesema kuwa sheria kali za usalama zilizowekwa,zinaashiria kutakuwa na udanganyifu mkubwa katika kuamua matokeo ya uchaguzi huo.
Hata hivyo serikali ya Zimbabwe imekanusha madai yote hayo na kuyaita hayana msingi.