Hariri awasili Paris, njiani kurudi Lebanon
18 Novemba 2017Kwa mujibu wa taarifa aliyoituma kwenye mtandao wake wa Twitter, Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema alizungumza kwa simu na Hariri mara tu baada ya kuwasili Paris, aliyemuhakikishia kuwa atarejea nyumbani siku ya Jumatano, ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu waziri mkuu huyo kujiuzulu akiwa Riyadh nchini Saudi Arabia.
Lebanon, ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa, inachukuliwa kama uwanja wa mapambano wa mataifa mengine yanayosaka ushawishi kwenye eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba ya Arabuni, zikiwemo Saudi Arabia na Iran.
Hariri aliwasili Paris na mkewe leo (Novemba 18) akitokea Saudi Arabia, na alitazamiwa kukutana na Rais Macron kwa mazungumzo yanayotarajiwa kutoa muelekeo wa hatima yake kisiasa.
Picha za televisheni zilimuonesha Hariri na mkewe wakiwasili bila watoto wao wawili, ambao inafahamika walikuwa nao pamoja nchini Saudi Arabia.
Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuwa watoto hao wamebakia kwa ajili ya mitihani ya skuli, ingawa wengine wanachukulia kubakia kwao kunazidisha mashaka juu ya endapo Saudi Arabia inahusika na njama za kumuondoa Hariri, mwenye pia uraia wa ufalme huo wa Ghuba.
Mzozo mpya Mashariki ya Kati?
Kujiuzulu kwa Hariri kulichukuliwa kama muakisiko wa shinikizo la Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia dhidi ya Iran na kundi la Hizbullah linaloungwa mkono na Iran ndani ya Lebanon.
Katika tamko lake la kujiuzulu, Hariri alisema alikuwa akihofia maisha yake, akizituhumu Iran na Hizbullah kwa kuifanya Lebanon na mataifa mengine ya Kiarabu yasiwe na amani.
Hata hivyo, Aoun na Hizbullah wamekuwa wakosoaji wakubwa wa Saudi Arabia kuhusiana na hatua hiyo ya Hariri kujiuzulu uwaziri mkuu akiwa huko, wakisema kuwa ufalme wa Saudia unahusika, huku Aoun akifika umbali wa kuituhumu serikali ya Mfalme Salman kwa "kumchukuwa mateka" Hariri.
Utawala wa Saudi Arabia unakanusha kuhusika na tangazo hilo la kujiuzulu, ukidai kuwa lilikuwa la Hariri mwenyewe na kwamba mwanasiasa huyo yuko huru.
Waziri mkuu huyo kutokea madhehebu ya Sunni amekuwa kiini cha uvumi tangu alipotangaza kujiuzulu tarehe 4 Novemba. Hatua hiyo ya ghafla imezusha mtikisiko na wasiwasi mkubwa wa kisiasa sio tu kwa Lebanon, bali pia eneo zima la Mashariki ya Kati.
Ufaransa ilikuwa ikishinikiza Hariri aweze kurudi Lebanon na kuweka wazi endapo anataka kweli kujiuzulu au kuendelea na wadhifa wake wa uwaziri mkuu, huku kwenyewe Lebanon wenzake serikalini wakisema kwamba hawakutambui kujiuzulu kwake.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/dpa
Mhariri: John Juma