1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Harris akubali kushindwa lakini arai "mapambano yaendelee"

7 Novemba 2024

Makamu wa Rais wa Marekani na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Kamala Harris ametoa hotuba ya kukubali kushindwa uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumanne.

Kamala Harris
Kamala Harris.Picha: Mike Blake/REUTERS

Pia amempongeza Donald Trump wa Republican kwa kuchaguliwa tena kuliongoza taifa hilo.

Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake mbele ya majengo ya Chuo Kikuu cha Howard mjini Washington, Bibi Harris amewarai wafuasi wake  "kutokata tamaa" akiwataka waendelee kupigania masuala yaliyochochea shauku yao wakati wa kampeni.

Harris ambaye kabla ya hotuba yake alimpigia simu Trump kukubali kushindwa na kumpongeza, amesema yeye na Rais Joe Biden watasaidia kufanikisha mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani.

Katika hatua nyingine, Rais Biden pia alizungumza na rais mteule Trump kwa njia ya simu ambapo amempongeza kwa ushindi aloupata kwenye uchaguzi wa Novemba 5 na kumkaribisha kuitembelea ikulu ya White House wakati akijiandaa kuchukua hatamu za uongozi.