1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harris na Blinken kuhudhuria mkutano wa usalama wa Munich

Josephat Charo
15 Februari 2024

Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris na waziri wa mambo ya nje Anthony Blinken wanakabiliwa na kibarua kigumu kuwahakikishia washirika kwamba Marekani bado imejitolea kwa dhati kuulinda usalama wao.

Rais Joe Biden, Kamala Harris an Antony Blinken
Rais Joe Biden atawakilishwa kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich na Makamu wake Kamala Harris, kushoto, na Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken, kulia.Picha: Shawn Thew/UPI/IMAGO

Harris na Blinken wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa usalama wa Munich chini ya wiki moja baada ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kusema hatawalinda washirika wa jumuiya ya kujihami NATO ambao watashindwa kutumia fedha za kutosha kwa ajili ya ulinzi.

Rais wa Marekani Joe Biden na Trump wako katika kinyang'anyiro kikali katika uchaguzi wa Novemba kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Reuters na shirika la Ipsos.

Biden ameamua kutohudhuria mkutano wa Munich katika miaka ya hivi karibuni lakini Harris amepangiwa hapo kesho kutoa kile ambacho wapambe wake wamekieleza kuwa ni hotuba kubwa kuhusu umuhimu wa kutimiza jukumu la Marekani la uongozo wa dunia, kabla kukutana na wabunge wa Marekani, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

Zelensky anasafiri leo kuja hapa Ujerumani kukutana na Scholz na baadaye atakwenda Ufaransa kukutana na rais Emmanuel Macron kabla kuelekea Munich ambako anatarajiwa kuuhutubia mkutano wa usalama siku ya Jumamosi.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amekuwa akiiwakilisha Marekani katika Mkutano wa Usalama wa Munich.Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Harris huenda akafuatiliwa kwa karibu kwa uwezo wake wa kuongoza baada ya ripoti ya wizara ya sheria wiki iliyopita kumueleza Biden mwenye umri wa miaka 81 kama mzee asiye na kumbukumbu nzuri. Trump ana umri wa miaka 77.

Mkutano wafanyika wakati Ulaya ikikabiliwa na vita

Mkutano wa Munich unafanyika wakati mzozo kati ya Urusi na nchi za Magharibi umeleta vita Ulaya, bara ambalo limetumia miongo kadhaa kudumisha amani, kupitia msaada wa Marekani kwa muungano wa kijeshi wa NATO ambao Trump ametishia kuachana nao.

Baraza la seneti la Marekani siku ya Jumanne liliidhinisha msaada wa dola bilioni 95.34 kwa ajili ya Ukraine na nchi nyingine, lakini msaada huo huenda usipigiwe kura katika baraza la wawakilishi kutokana na upinzani wa Trump.

Trump alitoa kauli wakati wa mkutano wa kisiasa katika jimbo la South Carolina Jumamosi iliyopita kuhusu kile alichokitaja kuwa ni malipo duni yanayofanywa na wachama wa NATO na kugusia mazungumzo aliyowahi kuyafanya na mkuu wa "nchi moja kubwa" kuhusu uwezekano wa kushambuliwa na Urusi.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, ndiyo atakuwa mwenyeji wa wakuu wa nchi watakaohudhuria mkutano wa Munich.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mkataba wa NATO una kipengee kinachohakikisha ulinzi kwa nchi wanachama iwapo mojawapo itashambuliwa.

Soma pia: NATO walaani kitisho cha Trump

Biden aliyakosa matamshi ya Trump kama mualiko kwa rais wa Urusi Vladimir Putin kuwashambulia wanachama wa NATO na akasisitiza umuhimu wa msaada wa dharura kwa Ukraine.

Jeremy Shapiro, Mkurugenzi wa utafiti katika Baraza la Ulaya kuhusu Mahusiano ya kigeni amesema hatarajii Kamala Harris au Blinken kutoa ahadi zozote katika mkutano wa Munich kuhusu kile ambacho kinaweza kufanywa na utawala wa Trump.

Shapiro amesema Harris na Blinken watatoa ujumbe rahisi; kwamba watashinda uchaguzi wa Novemba.

(reuters, afp, dpa)