1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa Bayern Harry Kane amaliza ukame wa mabao

18 Desemba 2023

Harry Kane amemaliza ukame wake wa kutofunga bao katika mechi tatu zilizopita baada ya kufunga mabao mawili na kuisaidia klabu yake ya Bayern Munich kuandikisha ushindi wa 3-0 dhidi ya Stuttgart.

Ligi Kuu ya Bundesliga I FC Köln vs Bayern München | Harry Kane
Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry Kane akisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya FC KölnPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Miamba hao wa Ujerumani walikuwa chini ya shinikizo kuelekea mchezo huo kufuatia ushindi wa 3-0 wa mahasimu wao msimu huu Bayer Leverkusen dhidi ya Eintracht Frankfurt, timu iliyoishushia Bayern Munich kichapo cha 5-1 wiki moja iliyopita.

Kufuatia ushindi huo, vijana wa Thomas Tuchel wamesimama katika nafasi ya pili kwenye jedwali wakiwa na alama 35, alama nne nyuma ya vinara wa Bundesliga Bayer Leverkusen, timu pekee ambayo bado haijafungwa msimu huu katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani.

Soma pia: Kane: Ni sharti tushinde mechi zilizosalia kabla mapumziko 

Baada ya kutoka sare ya 1-1 mfululizo katika mechi mbili zilizopita, Leverkusen iliandikisha ushindi wa 3-0 dhidi ya Frankfurt katika uwanja wa Bay Arena. Mabao ya Leverkusen yalitiwa wavuni na Victor Boniface, Jeremie Frimpong na Florian Wirtz.

Mechi za Bundesliga zitaendelea tena katikati ya wiki, wakati VfL Wolfsburg wakiialika Bayern Munich katika dimba la Volkswagen Arena nao vinara wa ligi Bayer Leverkusen wakiwa wenyeji wa VfL Bochum ugani Bay Arena.

Borussia Dortmund itakuwa na kibarua dhidi ya Mainz 05 huku Werder Bremen ikicheza na RB Leipzig.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW