1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harvard yapigwa marufuku kuandikisha wanafunzi wa kimataifa

23 Mei 2025

Hatua ya Marekani kuzuia Chuo Kikuu cha Harvard kuandikisha wanafunzi wa kimataifa imeibua taharuki ya kimataifa, huku chuo hicho kikisisitiza kwamba hakitokubali kushurutishwa na kufungua kesi dhidi ya utawala wa Trump.

USA Cambridge 2025 | Nembo ya Chuo Kikuu cha Harvard
Chuo Kikuu cha Harvard ni mmoja ya vyuo vya hadhi ya juu kabisaa duniani na hupokea maelfu ya wanafunzi kutoka kote duniani.Picha: Charles Krupa/AP/dpa/picture alliance

Hatua ya utawala wa Rais Donald Trump ya kuzuia Chuo Kikuu cha Harvard kuandikisha wanafunzi wa kimataifa imezua taharuki duniani kote, huku wachambuzi wakionya kuwa huenda ikawa na athari kubwa kwa taswira ya elimu ya juu ya Marekani. Harvard, mojawapo ya taasisi kongwe na zenye heshima kubwa duniani, imeitaja hatua hiyo kama kisasi cha kisiasa kisicho na msingi wa kisheria.

Kwa mujibu wa takwimu za chuo hicho, zaidi ya asilimia 27 ya wanafunzi wake kwa mwaka wa masomo 2024–2025 walikuwa kutoka nje ya Marekani. Marufuku hiyo sasa inatishia maisha ya kielimu ya maelfu ya wanafunzi, pamoja na mapato ya taasisi hiyo ambayo hutegemea ada kubwa kutoka kwa wanafunzi wa kigeni. Harvard imetangaza kuwa itatoa msaada wa kisheria kwa waliodhurika huku ikienda mahakamani kupinga hatua hiyo.

Katika taarifa yake ya kesi iliyowasilishwa Boston, Harvard imesema serikali imekiuka Katiba kwa kujibu kwa ukatili msimamo wa chuo hicho wa kutojihusisha na siasa za Ikulu. Harvard inadai kuwa hatua hiyo ya ghafla inafuta robo ya wanafunzi wake—takriban 7,000—na kudhoofisha msingi wa kimataifa wa taasisi hiyo. Pia inadai kuwa haikuwa na nafasi ya kujitetea kabla ya marufuku hiyo kutangazwa.

Wanafunzi na wanachama wa Harvard wakishiriki maandamano kupinga chuo hicho kuingiliwa kisiasa na utawala wa Trump.Picha: AP/dpa/picture alliance

Hofu na wasiwasi vimetanda zaidi miongoni mwa wanafunzi wa kimataifa, hasa kutoka China. Jennifer, mwanafunzi kutoka Beijing aliyepanga kuanza masomo yake nchini Marekani msimu huu wa vuli, alisema sasa hana uhakika wa mustakabali wake wa kielimu. Xiaofeng Wan, mshauri wa udahili wa vyuo, amesema amepokea simu nyingi kutoka kwa wazazi na shule mbalimbali wakihitaji ufafanuzi na msaada.

Serikali ya China imekosoa vikali hatua hiyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mao Ning, amesema kuwa siasa hazipaswi kuingizwa katika elimu, na kwamba hatua hiyo itaharibu taswira ya Marekani duniani.

"Ushirikiano wa kielimu kati ya China na Marekani unawanufaisha wote. China siku zote inapinga kisiasa kufanywa kwa ushirikiano wa kielimu. Njia hii ya Marekani itaathiri tu taswira na uaminifu wake kimataifa. China itatetea kwa uthabiti haki halali za wanafunzi na wasomi wake walioko ng'ambo."

Ujerumani yataka busara itumike

Wasiwasi huo umeenea hata Ulaya. Waziri wa Utafiti wa Ujerumani, Dorothee Baer, amesema ni jambo la kusikitisha kuona taifa lililojulikana kwa uhuru wa kielimu likifunga milango kwa vijana kutoka mataifa mengine. Baer aliongeza kuwa wanafunzi kutoka China, India na hata Marekani sasa wanageukia vyuo vya Ulaya ambako wanahisi haki zao zinalindwa zaidi.

Mashirika na taasisi za elimu pia zimechukua hatua. Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Hong Kong kimetoa mwaliko kwa wanafunzi waliokuwa wamejiandikisha Harvard, kikiahidi kuwasaidia kuhamia kwa haraka na kuwapa mazingira bora ya kujifunzia. Uamuzi huo wa Trump sasa unaonekana kusababisha mabadiliko ya haraka katika sifa ya Marekani kama kiongozi wa elimu ya juu.

Soma pia: Baada ya Harvard kukataa kuburuzwa, Trump aongeza vitisho

Tuhuma zilizotolewa na serikali ya Trump dhidi ya Harvard ni nzito. Zinajumuisha madai kuwa chuo hicho kimeunda mazingira yasiyo salama kwa wanafunzi wa Kiyahudi, pamoja na kushirikiana na Chama cha Kikomunisti cha China. Harvard imesema bado itajibu rasmi madai hayo ya wabunge wa Republican, lakini imesisitiza haitalegeza misingi yake ya kisheria na kitaaluma kwa hofu ya kisiasa.

Harvard: Matakwa ya serikali yanakiuka haki ya faragha

Chanzo cha hatua hii ni barua kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem, aliyedai Harvard iwasilishe rekodi zote za wanafunzi wa kimataifa, ikiwemo video na sauti za wale walioshiriki maandamano. Harvard imetaja shinikizo hilo kuwa kinyume na faragha na haki za kisheria za wanafunzi.

Hata familia za kifalme zimeathiriwa. Ikulu ya kifalme ya Ubelgiji imethibitisha kuwa Princess Elisabeth, mrithi wa kiti cha enzi, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili chuoni Harvard, sasa hatima yake iko njia panda kutokana na marufuku hiyo. Familia hiyo imesema inafuatilia kwa karibu kuona iwapo mwanao ataweza kurejea kwa muhula ujao.

Trump anataka kuilaazimisha Harvard ikubaliane na matakwa yake, lakini cho hicho kimesima kidete kupinga hatua hizo.Picha: Joseph Prezioso/AFP

Wachambuzi wa elimu wanasema marufuku hii ni sehemu ya mwelekeo mpana wa kisiasa wa Marekani chini ya Trump wa kulenga taasisi huru zinazoonekana kupingana na misimamo ya serikali. Harvard tayari ilikuwa kwenye mvutano na Ikulu kuhusu ufadhili wa dola bilioni 2 ambao ulisitishwa mapema mwaka huu.

Katika mazingira haya ya kisiasa na kiutawala, kesi ya Harvard inaweza kuwa kipimo cha mustakabali wa uhuru wa kielimu na nafasi ya Marekani kama kivutio kikuu cha kimataifa kwa wanafunzi na watafiti. Hatua ya mahakama sasa inasubiriwa kwa hamu, huku dunia ikitazama iwapo taasisi hiyo kongwe itafanikiwa kulinda misingi ya uhuru wa kitaaluma dhidi ya mashinikizo ya kisiasa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW