Hasara ya kiuchumi na uharibifu wa misitu
30 Mei 2008Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Sigmar Gabriel,kama rais wa mkutano huo mjini Bonn,ametoa wito kwa mawaziri wenzake wa mazingira kukubaliana njia ya kukomesha kutoweka kwa mimea na viumbe mbali mbali hapa duniani.Amesema:
"Haya ni matukio yatakayokuja kuwaathiri watoto na wajukuu wetu katika siku zijazo.Hiyo ni sababu ya kuuliza:Kiuchumi,uhai anuai una thamani gani?Hasara gani ya kiuchumi inasababishwa na kutoweka kwa mimea na viumbe mbali mbali?"
Hayo ni baadhi ya masuala yaliyowashughulisha wajumbe usiku mzima kwenye mkutano wa Bonn.Wajumbe hao wamejigawa katika makundi mbali mbali kujadiliana njia ya kuhifadhi misitu,bahari,matumizi ya maliasili na hata mada ya utata kuhusu mafuta ya kuendeshea magari yanayotokana na mazao ya kilimo na jinsi uhai anuai yaani uhusiano wa mimea na viumbe kutegemeeana, unavyoathirika.
Siku ya Alkhamisi Waziri Gabriel aliashiria kuwa makubaliano,yalioitwa "Mwongozo wa Bonn" yamepatikana juu ya njia ya kugawana faida zinazopatikana kutokana na mimea na viumbe mbali mbali.
Vile vile kama nchi 60 zimekubali kuunga mkono mradi wa mfuko wa kuhifadhi wanyama duniani-WWF kukomesha uharibifu wa misitu katika nchi za tropiki.Mada kuu iliyojadiliwa katika mkutano wa siku kumi na mbili imehusika na njia ya kuhifadhi misitu,ikitathminiwa kuwa asilimia 80 ya mimea na viumbe mbali mbali hukutikana misituni.
Siku ya Jumatano,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipofungua majadiliano ya kisiasa kwenye mkutano huo alisema,Ujerumani kati ya mwaka 2009 na 2012 itatoa kiasi cha Euro milioni 500 kusaidia kuhifadhi misitu iliyo katika hatari ya kutoweka.Na kuanzia 2013 Euro milioni 500 zingine zitatolewa kila mwaka kusaidia mradi huo.
Huu ni mkutano wa tisa wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhai anuai.Mkutano huo ulizinduliwa mwaka 1992 kwenye Mkutano wa Mazingira mjini Rio de Janeiro,Brazil.