1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hasara zaongezeka kutokana na majanga ya mabadiliko ya hewa

27 Desemba 2021

Gharama kutokana na majanga yaliyosababishwa na hali mbaya ya hewa mwaka 2021 ilikuwa zaidi ya dola bilioni 170.

Deutschland | Ahrweiler | nach dem Unwetter
Picha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Kulingana na shirika la misaada la Kikristo la Uingereza, hiyo ni dola bilioni 20 zaidi kuliko hali ilivyokuwa mwaka 2020. 

Kila mwaka, shirika hilo la Kikristo la misaada la Uingereza hufanya tathmini kuhusu hasara kutokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, mfano mafuriko, mioto na ongezeko la joto. Hayo yalitegemea ripoti ya maombi ya fidia yaliyowasilishwa na waathiriwa wa majanga hayo kwa mashirika ya bima.

Maoni: COP26 ni kikombe nusu na sio nusu kikombe

Katika mwaka 2020, shirika hilo lilibaini kwamba majanga 10 mabaya zaidi yaliyotokea ulimwenguni kutokana na mabadiliko ya hewa, yaligharimu dola bilioni 150 kushughulikia uharibifu.

Kwa kulinganisha na hasara ya mwaka huu ambayo ni dola bilioni 170, hiyo ni ongezeko la asilimia 13 kati ya mwaka jana na mwaka huu.

Shirika hilo la misaada, 'Christian Aid' limesema ongezeko hilo linaakisi athari zinazosababishwa na wanadamu wenyewe katika mabadiliko ya tabia nchi.

Rais wa Marekani Joe Biden alipozuru mitaa iliyoharibiwa na kimbunga Ida Septemba 7,2021 eneo la Manville.Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Euro milioni 400 kusaidia wahanga wa mafuriko Ujerumani

Kimbunga Ida kilisababisha hasara kubwa zaidi

Limeongeza kuwa watu wasiopungua 1,075 pia walipoteza maisha yao kutokana na majanga hayo kumi, na wengine milioni 1.3 walipoteza makaazi yao.

Janga lililokuwa na hasara ya juu zaidi mwaka 2021 ni kimbunga Ida kilichopiga Marekani na uharibifu wake uligharimu dola bilioni 65.

Baada ya kulipiga jimbo la Louisiana mwishoni mwa mwezi Agosti, kilisababisha pia mafuriko makubwa jimbo la New York City na viunga vyake.

Mafuriko mabaya yaliyoikumba Ujerumani na Ubelgiji mwezi Julai, ni janga lililoshika nafasi ya pili. Uharibifu wake uligharimu dola bilioni 43.

Vifo kutokana na mafuriko Ulaya vyapindukia 150

Kimbunga cha msimu wa baridi katika jimbo la Texas kilichosababisha jimbo hilo kupoteza nguvu ya umeme kilisababisha uharibifu uliogharimu dola bilioni 23. Kisha kikafuatwa na mafuriko yaliyoukumba mkoa wa Henan nchini China katika mwezi wa Julai. Uharibifu wa mafuriko hayo ulikadiriwa kugharimu dola bilioni 17.6.

Majanga mengine yaliyoorodheshwa kuwa miongoni mwa yaliyosababisha uharibifu wa kiasi kikubwa cha fedha ni pamoja na mafuriko ya Canada, baridi shadidi iliyokumba Ufaransa na kuharibu mimea, na vilevile tufani iliyotokea India na Bangladesh mwezi wa Mei.

Hasara za nchi maskini hazijajumuishwa

Ripoti hiyo inakiri kuwa tathmini yake huzingatia zaidi majanga katika mataifa tajiri, ambako kuna mpango mzuri wa bima kushughulikia uharibifu wa miundo mbinu.

Kwa maana hiyo ripoti hiyo imesadiki kuwa hasara kutokana na majanga kama hayo yanapotokea katika mataifa maskini, aghalabu haifanyiwi tathmini.

Ilitoa mfano wa Sudan Kusini ambako mafuriko yalitokea na kuwaathiri takriban watu 800,000.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa ''baadhi ya majanga mabaya kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliathiri zaidi nchi maskini, ambazo mchango wao katika athari za mabadiliko ya tabia nchi ni finyu''.

Mikasa ya moto ni miongoni mwa majanga yaliyoorodheshwa kusababisha hasara ya mabilioni ya dola.Picha: Cenk Gencdis/Depo Photos/abaca/picture alliance

Mnamo katikati ya mwezi Desemba, kampuni kubwa ya bima ulimwenguni Swiss Re, ilikadiria kwamba majanga asilia pamoja na yaliyosababishwa na hali mbaya ya hewa mwaka huu, yalisababisha uharibifu uliogharimu dola bilioni 250.

Ilieleza zaidi kwamba kiwango hicho kiliashiria ongezeko la asilimia 24 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Aidha, kulingana na kampuni hiyo, gharama hiyo kwa sekta ya kampuni za bima, ndiyo ilikuwa ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka wa 1970.