1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hassan Sheikh Mohamud arejea kuwa rais wa Somalia

16 Mei 2022

Rais wa zamani wa Somalia aliyeshindwa katika uchaguzi wa 2017 amerejea madarakani baada ya kumpiku rais wa sasa, katika kinyang'anyiro cha muda mrefu kilichoamuliwa na wabunge katika duru ya tatu ya upigaji kura.

Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Picha: Abukar Mohamed Muhudin/AA/picture alliance

Hassan Sheikh Mohamud, aliyehudumu kama rais wa Somalia kati ya mwaka wa 2012 na 2017, alishinda uchaguzi huo katika mji mkuu Mogadishu, wakati kukiwa ulinzi mkali uliowekwa na mamlaka ili kuzuia mashambulizi makali ya wanamgambo wa itikadi kali.

"Linapokuja suala la chuki za aina yoyote, niko tayari kuzitatua, kama tu nilivyosema wakati natangaza kugombea urais mwanzoni mwa wiki hii. Hakuna kisasi wala ufuatiliaji wa kisiasa unaomlenga mtu yeyote. Nchi hii ina kanuni na sheria za kutosha na kama tofauti zozote zikitokea, tutapitia sheria zilizotungwa na nchi hii." Amesema Mohamud.

Ushindi ni wa watu wa Somalia

Amesema ushindi huo ni watu wa Somalia, na huo ni mwanzo wa enzi ya umoja, demokrasia ya Somalia na mwanuzo wa vita dhidi ya rushwa. Aliongeza kuwa anaona kazi ngumu mbele baada ya kushinda urais.

Mohamed Abdullahi Mohamed akiri kushindwaPicha: Str/AFP

Duru ya kwanza ya upigaji kura ilikuwa na wagombea 36, ambapo wane walisonga hadi duru ya pili. Baada ya kukosekana mshindi aliyepata angalau theluthi mbili ya kura 328, upigaji kura kisha ukaingia katika duru ya tatu ambapo ushindi wa zaidi ya nusu ya kura ulitosha kumchagua mshindi.

Soma pia: Somalia yajiandaa kwa uchaguzi licha ya hofu ya usalama

Wajumbe wa mabaraza mawili ya bunge walimchagua rais katika kura ya siri iliyopigwa ndani ya katika uwanja wa ndege wa kambi ya jeshi ya Halane, ambayo inalindwa na walinda amani wa Umoja wa Afrika. Kuchaguliwa kwa Mohamud kumekamilisha mchakato wa uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu ambao uliibua mivutano ya kisiasa na ongezeko la wasiwasi wa ukosefu wa usalama, baada ya muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Mohamed kumalizika Februari 2021 bila kuwepo na mrithi wake.

Farmajoo akiri kushindwa

Mohamed, maarufu kama Farmaajo alikiri kushindwa, na Mohamud akaapishwa mara moja. Mohamud mwenye umri wa miaka 66, ni kiongozi wa chama cha Union for Peace and Development ambacho kina wingi wa viti katika mabaraza yote mawili ya bunge. Anatokea ukoo wa Hawiye, mojawapo ya koo kubwa kabisa Somalia, na anazingatiwa kuwa kiongozi wa taifa mwenye mtizamo wa upatanisho. Wasomali wengi wanatumai Mohamud anaweza kuiunganisha nchi baada ya miaka miwingi ya mivutano ya koo zilizogawika lakini pia kuchukua usukani thabiti wa serikali ya shirikisho ambayo ina udhibiti mdogo zaidi ya Mogadishu.

Wabunge wawili ni miongoni mwa watu 30 waliouawa katika mlipuko wa Machi 23 mjini MogadishuPicha: Hassan Ali Elmi/AFP/Getty Images

Wachambuzi walikuwa wamebashiri kuwa Mohamed angekabiliwa na vita vikali ili kuchaguliwa tena. Hakuna rais aliyeko madarakani ambaye amewahi kuchaguliwa kwa mihula miwili mfululizo katika taifa hilo la upembe wa Afrika, ambako koo pinzani hupigania vikali madaraka ya kisiasa. Katika kushinda uchaguzi huo hata hivyo, Mohamud ameweka historia kwa sababu hakuna rais wa zamani aliyewahi kufanikiwa kurejea madarakani.

Soma pia: Al-shabaab yashambulia kambi ya walinda amani wa AU

Lengo la kufanya uchaguzi wa moja kwa moja, wam tu mmoja kura moja nchini Somalia, nchi yenye watu milioni 16, bado gumu kwa kiasi kikubwa kutokana na mashambulizi makali ya itikadi kali. Maafisa walikuwa wamepanda kuwa na uchaguzi wa moja kwa moja mara hii lakini, badala yake, serikali ya shirikisho na majimbo wakakubali kuwa na "uchaguzi mwingine usio wa moja kwa moja,” kupitia wabunge waliochaguliwa na viongozi wa jamii – wajumbe wa koo zenye nguvu – katika kila jimbo mwanachama.

APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW