1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hata Rais wa Marekani Donald Trump hayuko juu ya sheria.

31 Julai 2020

Rais wa Marekani, Donald Trump alisema angetaka uchaguzi wa mwezi Novemba ucheleweshwe kwa muda wa miezi mitatu lakini baada ya kupingwa vikali hata na wanachama wa chama chake cha Republicans sasa abadilim kauli.

USA | US-Präsident Trump | PK im Rosengarten
Picha: Reuters/J. Ernst

Trump aliyasema hayo kwenye mtandao wa Twitter na kusema kuwa njia hiyo ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu itakuwa ni aibu kubwa kwa Marekani na hivyo akapendekeza kwamba uchaguzi ucheleweshwe ili watu waweze kupiga kura kwa salama. Lakini baadaye katika mkutano na waandishi wa habari Trump alisisitiza tena shaka yake juu ya mchakato wa uchaguzi.

Madai ya rais Trump yasiyo na ushahidi kwamba upigaji kura kwa njia ya posta, ikiwa ni njia ya kuwalinda wapiga kura dhidi ya janga la corona kutasababisha udanganyifu katika zoezi hilo. Cha kustaabisha rais huyo wa Marekani dakika chache baadae alibadili kauli yake na kusema wala sio nia yake kuuchelewesha uchaguzi.

Hata hivyo kauli yake ilisababisha hasara kwenye masoko ya hisa na iliudhoofisha uchumi wa Marekani hadi kufikia asilimia 32.9 hali mbaya katika kipindi hiki cha robo ya pili ikilinganishwa na hali ya uchumi ilivyokuwa katika kipindi cha robo ya kwanza. Uchumi umeteteleka na kuanguka hadi kufikia asilimia 9.5  tofauti na kipindi kama hicho cha mwezi wa Aprili hadi Juni mwaka jana.

Wachumi wanasema Marekani imeathirika pakubwa na hali hiyo imesababisha ukosefu wa ajira. Wakosoaji wamesema hali hiyo imetokana na usimamizi mbaya wa janga la maambukizi ya virusi vya corona na kwamba ndio sababu kubwa kwa nini Trump anakabiliwa na kitisho cha kushindwa katika uchaguzi utakaokuwa katika muda usiozidi siku 100.

Mgombea wa urais wa chama cha Democrats Joe BidenPicha: picture-alliance/dpa/AP/M. Rourke

Kura za maoni zinaonesha kwamba Trump atashindwa uchaguzi kutokana na kupoteza umaarufu wake. Trump, ambaye atapambana kwenye kinyang'anyiro hicho na mgombea wa chama cha Democrats Joe Biden ifikapo Novemba 3, hana mamlaka ya kikatiba ya kubadilisha tarehe ya kupiga kura, ambayo imeidhinishwa kisheria. Na kurudia kwake mara kwa mara wazo lake hilo, kunakiuka desturi ya marais wa Marekani na hatua hiyo imeongeza mvutano wakati huu ambapo vyama vya kisiasa nchini Marekani vinasuguana kuhusu namna ya kukabiliana na janga la corona.

Kamati ya kitaifa ya demokrasia imesema katika taarifa yake kwamba vtiisho vya Trump ni ishara kwamba amekata tamaa na hivyo anajaribu kuvuruga. Kamati hiyo imesema rais Trump anaweza kuandika kwenye Twitter yote anayotaka, lakini ukweli ni kwamba hawezi kuchelewesha uchaguzi, na Novemba ikifika, wapiga kura watamuadhibu.

Wanachama wa chama cha Republicans wanasema hawakubaliani na Trump na kwamba uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika kisheria na wala Marekani katika historia yake haijawahi kuruhusu kucheleweshwa, uchaguzi hata wakati wa vita isipokuwa ni bunge  peke yake ndiyo linaweza kubadilisha tarehe kupiga kura.

Wakati ambapo Baraza la Wawakilishi linadhibitiwa na chama cha Democrats na lile la Seneti linadhibitiwa na chama cha Republicans ni wazi kwamba kwa upinzani uliopo, wazo la Trump halitafika mbali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW