Hatari kwa wapelekaji misaada Somalia
27 Julai 2011Somalia inakabiliwa na janga la njaa lisilokuwa na mithili katika historia yake,nchi hiyo haina uwezo wa kukidhi mahitaji yake ya chakula pia kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mingi. Somalia ni nchi iliyoanguka.
Mashirika mbalimbali ya misaada yapo nchini Somalia kusaidia kuyaokoa maisha ya mamilioni ya watu waliomo katika hatari ya kufa njaa. Na shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa, limearifu kwamba huenda leo likaanza kuwapelekea watu wa Somalia misaada ya chakula kwa kutumia ndege.
Lakini aghalabu wanaoshiriki katika juhudi za kuwasaidia watu wa Somalia huyahatarisha maisha yao.
Sababu ni kwamba nusu ya Somalia inadhibitiwa na wapiganaji wenye itikadi kali za kiisalamu al Shaabab.
Sharifa Omar ni mfanyakazi wa Shirika la misaada la nchini Somalia na anaeleza kuwa wakati mwingine mtu hulazimika kufanya kazi kwa kujificha. Watu wengi wa al -Shaabab hawajui kusoma wala kuandika. Hawajui lolote juu ya mashirika ya misaada, yawe ya wasomali au kutoka nje. Na hata nembo haisaidii kitu. kwa hiyo huwa ni hatari.
Lakini Somalia imo katika hali mbaya sana kutokana na ukame na hakika inahitai misaada ya haraka. Watu wapatao milioni tatu na nusu wamo katika hatari ya kufa njaa.
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP leo linatarajia kuanza kuwapelekea watu hao msaada wa chakula na mahitaji mengine kwa kutumia ndege.
Ndege hizo zitaruka kutokea Kenya na kuyapeleka mahitaji mjini Mogadishu.
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa limesema kuwa baadhi ya ndege zao zitapeleka chakula katika mji wa Dolo nchini Ethiopia uliopo kwenye mpaka na Somalia.
Hata hivyo wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanapaswa kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa.Kwani ni hivi karibuni tu ,wafanyakazi wa shirika la Sharifa Omar Abukar waliuliwa na wapiganaji wa al -Shabaab .
Mwandishi/ Rühl Bettina/WDR/
Tafsiri/Mtullya abdu/
Mhariri/Abdul-Rahman