Hatari ya kuenea kwa sumu yapungua Hungary
8 Oktoba 2010Mto wa Danube, ambao ni mrefu zaidi barani Ulaya, sasa huenda ukawa hauko tena kwenye hatari ya maji yake yote kuenea sumu ya alkalini kama ambavyo hali ilianza kujionesha siku tatu zilizopita, (kuanzia Jumatatu ya tarehe 4 Oktoba 2010) pale matope yenye alkalini yalipoanza kuvuja kutoka kwenye kiwanda cha aluminium na kuingia kwenye mto huo.
Msemaji wa kikosi cha kupambana na majanga cha Hungary, Tibor Dobson, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba, jitihada za uokoaji zinakwenda vyema na kwamba hadi sasa mto wa Danube haujapata athari kubwa sana, kwani rekodi walizokusanya zinaonesha kwamba kiwango cha pH katika mto huo ni baina ya 8 hadi 8.2, ambacho si kibaya sana.
pH ni kipimo kinachotumiwa na wataalamu kupima kiwango cha tindikali na au alkalini kwenye maji. Kwa kawaida maji hutakiwa yawe na pH 7.0 ili yaitwe kuwa ni safi, lakini yanaitwa hatari yanapokuwa na ph 9 kwenda juu.
Alkhamis hii (7 Oktoba 2010) kulikuwepo na ripoti za kufa kwa samaki wengi katika mito ya Raba na Mosoni-Danube, ambako kiwango cha alkalini bado kilikuwa kiko juu ya ph 9. Katika mto mwengine wa mdogo wa Marcal, ambao ndio uliokuwa wa mwanzo kuvamiwa na sumu hii, samaki wote walikufa.
Hapo Jumanne (5 Oktoba 2010), serikali ya Hungary ilitangaza hali ya dharura katika majimbo matatu ya nchi hiyo, baada ya matope yenye kiwango kikubwa cha magadi kuyakumba maeneo ya Kolontar, Devescer na vijiji vyengine vilivyo umbali wa maili mia moja magharibi ya mji mkuu wa Budapest. Tayari watu wanne wameshafariki na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa kutokana na maafa haya.
Katika vijiji vilivyokumbwa na matope haya, vikosi vya uokoaji vinaendelea kusaidiana na wanajeshi na wanavijiji kusafisha maeneo yao na kuwatafuta watu watatu walipotea. Watu wengi wamepata matatizo ya kuungua ngozi na maradhi ya macho kutokana na kiwango kikubwa cha magadi kwenye matope hayo.
Hata hivyo, wataalamu wa mazingira wana matumaini kwamba janga hili linaweza kudhibitiwa na kwamba halitaweza kutoka nje ya mipaka ya Hungary, nchi iliyo katikati ya Bara la Ulaya. Mkurugenzi wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira la WWF, tawi la Hungary, Gabor Figeczky, ameiambia Reuters kwamba shirika lake linaamini, serikali ya Hungary inao uwezo wa kulidhibiti janga hili na kwamba hata maji ya mto yatakapofika mjini Budapest, yatakuwa yako salama.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman