Hatari ya kutokea mfumko wa bei kanda ya Asia
29 Aprili 2010Viongozi wa kanda hiyo wamehimizwa na IMF kurejea katika sera za kawaida ili kuzuia uwekezaji wa kubahatisha unaomiminika katika sekta ya uchumi. Ukuaji wa kiuchumi unaotazamiwa kuendelea katika nchi za Asia na tofauti kubwa ya riba iliyopo kati ya nchi hizo na zile zilizoendelea kiviwanda,huenda ikavutia mitaji zaidi katika eneo hilo.
Lakini hapo kuna hatari ya uchumi kukua haraka na kusababisha mfumko wa bei,pakiwepo uwezekano wa ukuaji huo kusita ghafla, imeonya ripoti iliyotolewa na tawi la IMF linaloshughulikia eneo la Asia na Pasifiki.Mkurugenzi wa idara hiyo,Anoop Singh amesema,China na nchi zingine katika kanda hiyo ya Asia,zihakikishe kuwa uwekezaji wa pupa usije ukamalizikia kwa kuporomoka ghafla uchumi,kama ilivyowahi kutokea hapo awali.
IMF inatathmini kuwa uchumi katika kanda ya Asia, mwaka huu wa 2010 na hata mwakani,utakua kwa asilimia 7.1 - hiyo ikiwa ni zaidi ya vile ilivyotabiriwa juma lililopita. Lakini shirika hilo la fedha pia limeonya kuwa uchumi wa nchi za magharibi unaokua pole pole kuliko ilivyotarajiwa, huenda ukaathiri uchumi wa kanda ya Asia unaotegemea mauzo ya nje. Kwa hivyo itakuwa busara kwa serikali za eneo hilo kutotegemea sana biashara yake ya nje na badala yake zichukue hatua za kuinua biashara ya ndani.Marekebisho muhimu yanahitaji kufanywa ili kuimarisha mashindano katika sekta za huduma.
Wakati huo huo,serikali hizo zinahitaji kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kuna uwiano katika matumizi ya fedha na biashara ya nyumba.Njia mojawapo ni kuregeza viwango vya kubadilisha fedha. Bila ya China kutajwa kwa jina, ripoti ya IMF imesema, uwekezaji wa muda mfupi unaweza kuzuiliwa kwa kupandisha kiwango cha kubadilisha fedha.Kwa mujibu wa IMF,fedha za kigeni zitaendelea kumiminika katika kanda ya Asia ikiwa thamani ya sarafu haitopandishwa zaidi.Hata hivyo,sarafu madhubuti pekee haitosaidia kuleta uwiano katika uchumi wa China na nchi zingine za kanda hiyo,aliongezea Anoop Singh. Amesema,serikali za eneo hilo la Asia zinahitaji pia kuongeza matumizi yake badala ya kuweka akiba.Hata mashirika makubwa nchini China na kwengineko katika kanda hiyo, yanapaswa kufanya hivyo.
Mwandishi: P.Martin/AFPE
Mhariri: Mwasimba,Saumu