1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hati ya kusafiri ya corona yatatizwa na kirusi cha Delta

1 Julai 2021

Hati ya kusafiri ya Covid-19 ya Umoja wa Ulaya imeanza kutekelezwa, kipindi cha likizo cha majira ya joto Ulaya, lakini aina mpya ya kirusi kinachosambaa kwa haraka cha Delta tayari inatishia kupunguza matumizi yake.

Bildergalerie über die Varianten des neuen Coronavirus
Picha: Christian Ohde/imago images

Hati hiyo ya Umoja wa Ulaya iliyo na nambari ya kuthibitisha inayopatikana kwenye simu au karatasi inaonyesha kama mwenye hati hiyo amechanjwa na moja ya chanjo zilizoidhinishwa na umoja huo za BioNTech/Pfizer, AstraZeneca, Mordena ama Johnson & Johnson, au wamepata nafuu baada ya kuambukizwa au wamepimwa na hawakupatikana na maambukizi. Soma zaidi Merkel, Johnson kujadili vikwazo kuepusha Covid-19

Chini ya sheria ya Umoja wa Ulaya, cheti hicho kinakusudiwa kumaliza hitaji la karantini au upimaji zaidi wakati wa kusafiri kati ya nchi 27 za Umoja wa Ulaya au mataifa manne yanayohusiana na Ulaya ya Iceland, Norway, Uswisi na Liechtenstein.

Nchi zote wanachama za Umoja wa Ulaya ziliunganishwa na mfumo wa cheti cha kidijitali siku ya Alhamisi isipokuwa Ireland, ambayo ilikumbwa na shambulio la kimtandao lililolenga huduma yake ya afya mnamo Mei, na ina mpango wa kuanza kazi tena mnamo Julai 19. soma  Corona: Kuchanganya dozi mbili tofauti za chanjo kunaimarisha kinga

Lakini kuongezeka kwa kirusi cha Delta, kilichogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini India na sasa kinasambaa kwa haraka kwengineko, kinaweza kusababisha "usitishaji wa dharura " wa kukubalika kwa cheti hicho.

Tayari Ujerumani imepiga marufuku wasafiri wanaoingia kutoka Ureno, ambapo kirusi cha Delta kimeathiri taifa hilo pakubwa. Raia au wakaazi wake pekee ndio wanaoruhusiwa kuingia kutoka Ureno, na lazima wakae karantini kwa wiki mbili baada ya kuwasili.

Uamuzi wa Ujerumani umeibua hasira kwa Umoja wa Ulaya, huku Kamishna wa Sheria wa umoja huo Didier Reynders akisema kwamba wanapaswa kuepuka marufuku ya kusafiri ndani ya Umoja wa Ulaya na kusisitiza kwamba Ujerumani ilipaswa kushauriana na washirika wake kwanza.

Kirusi cha Delta chasambaa kwa haraka

Kuanza kusambaa kwa kirusi cha Delta nchini Uingereza, na kiwango cha maambukizi ya wiki mbili yakiwa zaidi ya mara saba katika nchi wanachama wa Umoja Ulaya kunaibua wasiwasi mkubwa barani Ulaya. 

Wiki hii, Ureno, Uhispania na Malta wameongeza vizuizi kwa wasafiri kutoka Uingereza, ingawa nchi hizo tatu zilisema wataruhusu Waingereza waliochanjwa kikamilifu. 

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO siku ya Alhamisi limeonya kuwa idadi ya visa vya Corona vimeongezeka tena Ulaya, kufikia asilimia 10 baada ya kupungua miezi miwili iliyopita kutokana na kulegezwa kwa vizuizi vya kutangamana na kuongezeka kwa safari. 

Katika barua ya shirika la ushauri wa utafiti wa uchumi la Capital Economics imesema "Hakuna shaka kwamba idara ya utalii inaweza kuimarika wakati kwa msimu wa joto." Lakini ilitabiri cheti hicho kitakuwa na athari ndogo sana kwa utalii wa Ulaya mwaka huu, ikizingatia kwamba watu wazima wengi hawajachanjwa kikamilifu na kirusi cha Delta kinawafanya watu na serikali kuwa waangalifu zaidi.

Msongamo katika viwanja vya ndege

Picha: Getty Images/T. Lohnes

Mashirika ya ndege yaliyokusanyika pamoja chini ya kundi la ushawishi  la A4E, wameelezea wasiwasi wao kuwa njia isiyo sawa kati ya nchi za Umoja wa Ulaya katika kukagua cheti hicho cha Corona inaweza kuweka foleni ndefu katika viwanja vya ndege na kuna uwezekano wa kuibua hatari mpya za kiafya.

Aidha mashirika hayo ya ndege yametoa wito wa kutaka vyeti kukaguliwa mtandaoni kabla ya wasafiri kufika katika kiwanja cha ndege.

Kumekuwa na matatizo mbalimbali, katika uwanja wa ndege wa Brussels siku ya Alhamisi ambayo ni siku ya kwanza kurudi shule baada ya likizo ya msimu wa kiangazi Ubelgiji, na mgomo katika uwanja wa ndege Ufaransa pamoja na kuongezeka kwa ukaguzi wa Corona. Soma  Afrika yakabiliwa na wimbi la 3 la corona

"Kila kitu kimezuiwa," mfanyakazi mmoja alisema katika dawati la kuangalia ndege la Brussels, wakati safu kubwa ya abiria ikielekezwa kwenye hema la kusubiri ambapo ilani ya kuwekeana umbali kati ya mtu na mtu haikuzingatiwa.

"Tutaachwa na ndege ," familia moja yenye watoto wawili ililalamika.

"Hiyo ni Corona, huo ndio utaratibu. Ukikosa ndege yako, tunakupatia nyingine." alijibu mfanyakazi wa ndege.

Kwa ujumla serikali za Umoja wa Ulaya zinapima hamu ya umma ya mapumziko wakati huu wa msimu wa kiangazi dhidi ya harakati ya kutoa chanjo na kirusi cha Delta.

Takwimu za AFP zinazojumuisha data rasmi za kiafya kutoka Umoja wa Ulaya zinaonyesha kuwa asilimia 50.4 ya idadi ya watu wa nchi wanachama kufikia sasa wamepokea angalau dozi moja ya chanjo, ikilinganishwa na asilimia 66 nchini Uingereza. Hadi sasa, mtu mmoja kati ya watatu katika nchi ya Umoja wa Ulaya anachukuliwa kuwa ameshakamilisha dozi yote ya chanjo.

AFPE     

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW