1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Hans-Georg Maaßen Magazetini

Oumilkheir Hamidou
18 Septemba 2018

Hatima ya mwenyekiti wa idara ya upelelezi wa ndani Hans-Georg Maaßen, uvumi kuhusu uchaguzi wa kabla ya wakati nchini Uingereza na uchunguzi wa maoni ya wajerumani kuelekea wahamiaji ni miongoni mwa mada magazetini.

Hans-Georg Maaßen
Picha: picture-alliance/dpa/M. Murat

Tunaanzia Berlin ambako hii leo viongozi wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano wanatarajiwa kukutana na kuamua kama mwenyekiti wa idara ya upelelezi wa ndani Hans- Georg Maaßen aendelee na wadhifa wake au la. SPD wanashikilia mwenyekiti huyo ang'atuke, waziri wa ndani Horst Seehofer ambae ni mwenyekiti wa chama cha CSU anapinga . Gazeti la "Oberhessische Presse" linachambua jinsi kadhia hiyo inavyoitikisa serikali kuu ya muungano na kuandika: "Siwezi tena kufanya kazi na bibi huyu" amenukuliwa waziri wa ndani Horst Seehofer akisema mwezi juni uliopita."Bibi huyu alikuwa akimaanisha kansela Angela Merkel. Tangazo lake la kujiuzulu alilolitoa wakati ule na baadae kulibatilisha, lingekuwa jibu linalofaa.

Sasa hali ya mambo inaashiria malumbano mengine yatazuka kati ya Angela Merkel na Horst Seehofer. Waziri wa mambo ya ndani anamuunga mkono mwenyekiti wa idara ya upelelezi, huku SPD wakidai ang'atuke. Inasemekana kansela Merkel  anaunga mkono  pia fikra hiyo. Hata hivyo kansela anaamini mvutano huo hautakuwa sababu ya kuvunjika serikali kuu ya muungano. Ndio kusema ana karata zozote nyengine za kuufumbua mzozo huo? "

Uvumi wa kuitishwa uchaguzi kabla ya wakati Uengereza

Nchini Uingereza kuna uvumi huenda mvutano kuhusu Brexit ukasababisha uchaguzi mkuu kuitishwa kabla ya wakati. Gazeti la "General-Anzeiger" la mjini Bonn linaandika: "Eti uchaguzi wa kabla ya wakati utaleta ufumbuzi  kweli ikiwa mfuasi wa siasa asilia za mrengo wa kushoto, mpinzani wa Umoja wa Ulaya, Jeremy Corbyn atagombea kwa tikiti ya chama cha Labour na mwanasiasa anaefuata msimamo mkali kuelekea suala la kujitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya Brexit, Boris Johnson akiwania kwa tikiti ya wahafidhina?

 Wote wawili wanaigawa vibaya sana  jamii nchini Uingereza. Uchaguzi wa kabla ya wakati hautasaidia chochote na hata makubaliano ya kujitoa katika umoja wa ulaya Brexit hayatasaidia kitu. Watakaokula hasara zaidi hapo si wengine isipokuwa wananchi wa Uingereza."

Wajerumani hawana shida na wahamiaji

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha Ujerumani ambako utafiti wa maoni umedhihirisha asili mia 90 ya wajerumani wanasema hawana shida na wahamiaji. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika: "Utafiti huo umedhihirisha Ujerumani mashariki, ambako idadi ya wahamiaji ni ndogo, watu wanakerwa zaidi na wahamiaji. Kwa hivyo ile hali ya kutokujua ndio inayowafanya wawe na wasi wasi.Yeyote lakini anaeketi shuleni pamoja na Laila au Nehad hakosi kugundua mshikamano ulioko licha ya tamaduni tofauti. Na kwamba mazungumzo ni muhimu ili kuweza kuelewana."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(Inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW