1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya mkopo wa benki ya dunia kwa Tanzania haijulikani

30 Januari 2020

Serikali ya Tanzania imesema mvutano uliopo kati yake na Benki ya Dunia iliyozuia mkopo wa dola milioni 500 utamalizika tu. Waziri wa elimu nchini humo, amesema taifa linatumai benki hiyo itafikiria upya uamuzi wake.

Symbolbild | Geld | Umschlag
Picha: imago images/teamwork/A. Duwentäster

Waziri Ndalichako ambaye alikuwa akizungumza na wanafunzi wa shule moja ya sekondari jijini Dar es salaam amesema upepo unaoendelea kuvuma kuhusu sakata hilo utafikia tamati tu.

Huku akibainisha mipango ya serikali katika kutaka kuboresha elimu pamoja na kuwawekea mazingira mazuri kwa watoto wa kike, amesema uamuzi uliochukuliwa na benki hiyo ya dunia haumanishi kwamba jambo hilo limefikia tamati.

Ameeleza hatua ya serikali kutaka kukopa katika benki hiyo ya dunia uliotokana na majadiliano ya muda mrefu ambayo yaliridhiwa na pande zote hasa baada ya Tanzania kuwasilisha mapendekezo yake baada ya kufanya utafiti kuhusu uboreshaji wa sekta ya elimu.

Kulingana na nyaraka za Benki ya Dunia, mkopo huo pamoja na mambo mengine, ulikusudiwa kwenda kusaidia upatikanaji wa elimu bora na kwa urahisi kwa wanafunzi waliokuwa wanarudi shule baada ya kuwa wamepata ujauzito

Wanaharakati wa Tanzania walaumiwa kwa kukosa uzalendo

Picha: DW

Kwa hivi sasa kumekuwa na mjadala mkubwa unaendelea baada ya Benki ya Dunia kuahirisha upigaji kura kuhusu mkopo wa dola milioni 500 zilizokuwa zikilenga miradi mbalimbali ya elimu..

Kura hiyo ilikuwa imepangwa ipigwe siku ya Jumanne, lakini kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya benki hiyo iidhinishe mkopo huo kwa Tanzania ama la.

Taarifa za kuahirishwa kwa kura hiyo zilikuja siku chache baada ya shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa waliokuwa wakiitaka benki hiyo isitoe mkopo huo kwa serikali kutokana na kile walichokiita kuwa ni sera na sheria ya elimu ya kibaguzi.

Waziri Ndalichako amewalaumu wanaharakati wa Tanzania juu ya kile alichokiita kukosa uzalendo kutokana na hatua yake ya kuishinikiza benki ya dunia kusitisha mkopo huo. Miongoni mwa wale wanaotaja kuwa mstari wa mbele kuweka shinikizo hilo ni mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye pia ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo.

Zitto ambaye kwa sasa yuko ziarani katika nchi za magharibi ametetea msimamo wake huko na jana wakati akizungumza na shirika la habari la BBC Mjini London alikuwa na haya ya kusema.

Sheria ya elimu ya Tanzania inakipengele cha nidhamu ambacho kinatamka kuwa wasichana wanafunzi wanaogundulika kuwa na ujauzito wafukuzwe shule. Nyaraka kutoka Benki ya Dunia, zinaonyesha kuwa wanafunzi wa kike zaidi ya 5,000 walisimamishwa masomo mwaka mwaka 2017 baada ya kugundulika kuwa na ujauzito.

Chanzo: George Njogopa DW Dar es Salaam