1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya waziri mkuu Theresa May Magazetini

Oumilkheir Hamidou
25 Machi 2019

Kitandawili cha Brexit, na hatima ya waasi wa itikadi kali wa IS baada ya ngome yao ya mwisho Baghouz kuporomoka ni miongoni mwa mada zilizomulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

London Theresa May Premierministerin Großbritannien
Picha: picture-alliance/empics/J. Brady

Tunaanzia Uingereza ambako homa ya Brexit inazidi kupanda na waziri mkuu Theresa May akitiwa kishindo na chama chake mwenyewe cha Tory ang'atuke. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: "Kuna kila ishara zinazoonyesha siku za mkuu wa chama cha Tory zinakaribia mwisho. Akijiuzulu kwa khiari au kwa kulazimishwa haitomaanisha kwamba tatizo litamalizika au vurugu za mchakato wa Brexit kuepukwa. Labda misimamo ya pande tofauti ingelainika.

Kwasababu kishindo cha mpango wa kutaka kujitoa katika Umoja wa Ulaya, kinachukua sura ya kishindo cha wabunge. Kwa kuwakaripia hivi karibuni wabunge, waziri mkuu Theresa May amejizidishia mashaka na kuwafanya wengi wamgeukie katika wakati ambapo tokea hapo hawakuwa wakimuunga mkono. May hana ujanja. Karata zote ameshazicheza. Kilichosalia ni kutaraji atakaekamata nafasi yake atafanikiwa angalao kuleta utulivu katika mchakato wa Brexit."

Brexit itageuka kuwa funzo kwa wengine

Gazeti la mji mkuu "Berliner Morgenpost" linazungumzia mafunzo yanayotokana na kishindo cha Brexit na kuandika: "Theresa May hakufanikiwa hata nukta moja .Kwa hivyo siku zake kama waziri mkuu zinamalizika. Mapinduzi ndani ya chama chake yakifanikiwa, atalazimika kujiuzulu . Vurugu la Brexit huenda likawa funzo kwa mataifa mengine wanachama wa Umoja wa ulaya. Hakuna yeyote anaejinata kupigania siasa za kizalendo atakaekwenda umbali wa kutaka kuitoa nchi yake katika Umoja wa ulaya akizingatia vishindo vya Brexit. Litakuwa funzo pia kwa Umoja wa ulaya wenyewe kuona baada ya Brexit, jinsi waingereza wataklavyokuwa."

Ngome ya mwisho ya IS yavunjwa

Na ripoti yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Syria. Ngome ya mwisho ya wafuasi wa itikadi kali wanaojiita "Dola la kiislam"IS, imekombolewa linaandika Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linalozungumzia kuhusu hatima ya wanamgambo wenye asili ya Ujerumani: "Kwa Ujerumani walikotokea wafuasi 1000 wa IS walioelekea katika maeneo ya vita , hakuna kinachosaidia si  kujaribu kufifiisha mambo na wala  si kuyakuza. Kinachohitajika ni kuwa waangalifu pamoja na kuendelezwa ushirikiano pamoja na taasisi za usalama katika maeneo hayo ya vita ili kuhakikisha wapiganaji wa zamani wa IS hawarejeshwi hivi hivi nchini Ujerumani. Na hata kama itakuwa vigumu, lakini ihakikishwe waliofanya maovu miongoni mwa watu hao wanafikioshwa mahakamani nchini Ujerumani.

 

MwandishiHamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW