1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimae Omanyala asema atashiriki mashindano ya Oregon22

14 Julai 2022

Ferdinand Omanyala Mwanariadha mweye kasi zaidi Afrika amesema ana matumaini ya kushiriki mashindano ya riadha ya dunia huko Marekani licha ya kuchelewa kupata viza ya kumuwezesha kusafiri saa 24 kabla ya shindano hilo

Leichtathletik | Afrikameisterschaft Mauritius 2022
Picha: Deji Ogeyingbo

Omanyala anaeshiriki mbio za mita 100 awali alitangaza kuwa hatofanya hivyo kwa sababu ya kutopata viza hiyo kwa wakati. Mbio hizo ni sehemu ya mashindano yanayofanyika mjini Eugene katika jimbo la Oregon Marekani yatakayoanza asubuhi kuanzia saa tatu saa za Marekani. "Naabiri ndege Ijayo kwenda Oregon, naamini nitashiriki, asanteni sana kwa uungaji mkono wenu pamoja na maombi" alisema Omanyala katika mtandao wake wa Twitter baada ya kukabidhiwa cheti chake cha kusafiria.

Kulingana na wizara ya michezo ya Kenya mwanariadha huyo anatarajiwa kuondoka Kenya saa kumi na mbili jioni huku baadhi ya magazeti nchini humo yakikadiria kuwa iwapo safari yake itakwenda kama alivyopanga basi atatazamiwa kufika  Oregon masaa matatu au mawili kabla ya mbio hizo kuanza.

Msemaji wake aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Omanyala, alipokea viza yake Alhamisi akisema huenda kucheleweshwa huko kumetokana na mrundiko wa maombi ya kupata visa uliosababishwa na janga la COVID 19. Shirika la habari la Reuters limejaribu kupata maoni juu ya hili kutoka kwa shirika la wanariadha Kenya pamoja na Ubalozi wa Marekani lakini hadi sasa hawajafanikiwa.

Omanyala hatoshiriki mashindano ya riadha ya dunia Marekani

Mwaka uliyopita, Omanyala aliweka rekodi ya Afrika kwa wanaume kwa kukimbia kwa sekunde 9.77 katika shindano lililofanyika Nairobi, Kenya. Kijana huyo wa miaka 26 alishinda mashindano ya riadha ya Afrika ya mbio za mita 100 mwezi uliopita na alikuwa Mkenya wa kwanza kufuzu semi fainali ya mbio za mita 100 katika mashindano ya kombe la dunia mjini Tokyo mwaka uliopita.

Ferdinand Omanyala amesema atashiriki pia mashindano ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika mjini Birmingham uingereza kuazia tarehe 28 Julai hadi tarehe 8 Agosti mwaka  2022. Mwanariadha huyu ndiye mtu wa tatu mwenye kasi zaidi duniani akiwa nyuma ya Wamarekani Fred Kerley na Trayvon Bromell.

Chanzo: afp, reuters,ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW