1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Hatimaye Blinken akutana na Xi katika ziara yake ya Beijing

Sylvia Mwehozi
19 Juni 2023

Rais wa China Xi Jinping amekutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken ambaye yupo ziarani akijaribu kupunguza mivutano inayozidi kuongezeka baina ya mataifa hayo mawili.

China | Marekani
Waziri Antony Blinken na Rais Xi JinpingPicha: Li Xueren/Xinhua/IMAGO

Ziara ya Blinken nchini China iliyoanza Jumapili ni ya kwanza kwa afisa wa ngazi ya juu wa Marekanikatika kipindi cha takribani miaka mitano, ikikusudia kuhakikisha kwamba migogoro iliyopo baina ya mataifa hayo mawili, haigeuki kuwa vita.

Hatua ya Rais Xi kufanya mazungumzo na Blinken, inatizamwa kama ishara muhimu kwamba Beijing ina dhamira ya kupunguza joto la mivutano ya mataifa hayo mawili. Rais Xi amemweleza Blinken kwamba anatumai ziara yake itakuwa na "mchanga chanya" wa kuimarisha mahusiano baina ya Beijing na Washington.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Blinken aanza ziara China

Shirika la utangazaji la China CGTN limemnukuu Xi akisema kwamba "mazungumzo kati ya nchi na nchi yanapaswa kuzingatia kuheshimiana na ukweli. Ninatumai kuwa waziri Blinken kupitia ziara hii anaweza kutoa mchango chanya katika kuleta utulivu wa uhusiano kati ya China na Marekani."

Aidha, Rais Xi ameongeza kuwa upande wa China umeweka wazi msimamo wake na pande hizo mbili zimekubaliana kufuata maelewano ya pamoja ambayo Rais Biden na Xi walikuwa wamefikia huko mjini Bali, Indonesia, na kwamba "pande mbili pia zimepiga hatua na kufikia makubaliano juu ya baadhi ya masuala maalum."

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi Picha: LEAH MILLIS/REUTERS

Mazungumzo ya Xi na Blinken yamefanyika baada ya mwanadiplomasia huyo kufanya mazungumzo ya zaidi ya saa 10 na wanadiplomasia waandamizi wa China. Mapema siku ya Jumatatu Blinken alikutana na Mwanadiplomasia mkuu wa sera za nje za China Wang Yi ambaye ndani ya chama cha kikomonisti wadhifa wake unapita nafasi ya waziri wa mambo ya nje. Yi amemweleza Blinken kwamba ziara yake "inafanyika katika wakati muhimu wa mahusiano ya China na Marekani".Blinken atua Beijing kwa ziara ya ngazi ya juu

"Ni lazima kuchagua kati ya mazungumzo na makabiliano, ushirikiano au mzozo" alisema mwanadiplomasia mkuu wa China Yi, akiongeza kwamba ni lazima kubadilisha mwelekeo wa uhusiano unaodorora kati ya China na Marekani, kushinikiza kurejea kwenye njia yenye afya na utulivu, na kufanya kazi pamoja kutafuta njia sahihi ya China na Marekani kupatana." Kuhusu suala la Taiwan, Yi alisema kwamba "China haina nafasi ya maelewano au kukubali kushindwa".

Blinken kwa upande wake alisisitiza umuhimu wa mawasiliano ya wazi ili kusimamia  ushindani baina ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali vya China, Yi ameitaka Marekani kuacha kutoa vitisho kwa China, kuachana na "ukandamizaji" wake wa sayansi na maendeleo ya kiteknolojia ya China na kujiepusha na kuingilia kati mambo yake ya ndani.

Siku moja kabla, Blinken alikuwa tayari amekutana na waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gangkatika mazungumzo yaliyoelezwa na Washington kuwa yalikuwa ya "wazi na ya kujenga".