Hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yapata serikali
26 Agosti 2019Katika serikali hiyo mpya,Chama cha rais wa zamani Joseph Kabila kimechukuwa wizara muhimu zikiwemo sheria, ulinzi, fedha na akiba. Serikali hiyo ilitangazwa saa kumi na moja asubuhi ya leo 26.08.2019 baada ya kusubiriwa usiku mzima. Tangazo la serikali hiyo lilitolewa ikulu moja kwa moja kupitia runginga ya taifa. Serikali hiyo mpya inamawaziri 66 pamoja na waziri mkuu. Rais Tshisekedi alichelewesha kutangazwa kwake kutokana na kwamba alitaka kuwapo na waziri anayewawakilisha walemavu.
Kwenye serikali hiyo, vuguvugu la FCC, la rais wa zamani, Joseph Kabila limepata mawaziri 42, wakiwemo wale wa Sheria, ulinzi, fedha, madini, akiba na mipango ya serikali, huku vuguvugu la CACH la rais Tshisekedi likishikilia wizara ya mambo ya ndani, wizara ya mambo ya nje na bajeti.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kongo, mwanamke ataongoza wizara ya mambo ya nje. Mwanamama huyo Marie Ntumba Nzenza anatoka chama cha UDPS cha rais Thisekedi lakini hajulikani na waliowengi nchini humo.
Serikali hii itakuwa na manaibu watano wa mkuu akiwemo Elysee Munembwe kutoka FCC ambae ataongoza wizara ya mipango ya serikali, na Jean Baudouin Mayo katibu mkuu wa chama cha UNC cha Vital Kamerhe aliyeteuliwa kuwa naibu waziri mkuu anayehusika na bajeti.
Hata hivyo serikali hiyo ina idadi chache ya wanawake, kwa jumla ni aslimia 17 pekee ya wanawake. Wakaazi wa Kinshasa wamepongeza kuweko na serikali ambayo ina sura mpya na hasa vijana
Miongoni mwa mawaziri waliokuwa kwenye serikali ya Kabila na waliobahatika kurejea kwenye serikali hii mpya ni pamoja na Azarias Ruberwa waziri wa majimbo na Thomas Luahaka waziri wa elimu ya vyuo vikuu.
Majimbo yote 26 yamewakilishwa kwenye serikali hiyo. Aliy ekuwa gavana wa kivu ya kaskazini, Julien paluku ameteuliwa kuwa waziri wa viwanda. Ifahamike pia kwamba serikali hii ya rais Tshisekedi haikuwashirikisha wapinzani.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo, DW Kinshasa.