1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Edgar Lungu kuzikwa Afrika Kusini

Bryson Bichwa
24 Juni 2026

Mgogoro kuhusu mahali pa mazishi ya aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, umefikia mwisho baada ya familia ya kiongozi huyo wa zamani kushinda kesi dhidi ya serikali ya Zambia katika mahakama ya rufani ya Afrika Kusini.

 Sambias Präsident Edgar Lungu (2016)
Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu Picha: Philippe Wojazer/Reuters/Pool/picture alliance

Hatua hiyosasa inafungua njia kwa mazishi kufanyika nchini Afrika Kusini kama ilivyosisitizwa na familia ya marehemu.

Kufuatia uamuzi huo, familia ya Lungu sasa imesema inaingia rasmi katika kipindi cha maombolezo,baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mvutano wa kisheria uliokuwa ukihusu mahali pa kupumzishwa kwa kiongozi huyo wa zamani kama anavyofafanua msemaji wa familia ya Lungu Jonas Zimba.

"Kwa familia ya Lungu, maana yake ni kwamba sasa tumefikia mwisho wa mzozo huu. Tumekuwa tukihangaika na suala hili kwa karibu mwaka mmoja na zaidi. Kwa sasa, mzozo umeisha na familia imeanza rasmi kipindi cha maombolezo. Serikali ya Zambia imesema haikubaliani na uamuzi huo, lakini haitapinga hukumu ya Mahakama ya Rufani. Hivyo kwa sasa, hakuna mgogoro tena.”

Zambia pia ameizungumzia hali ya uhusiano kati ya familia na serikali, akisisitiza kuwa hakuna mivutano inayotarajiwa kuendelea kutokana na uamuzi huo wa mahakama.

"Familia ya Lungu bado ni raia wa Zambia, na kama raia hakuna tatizo na serikali yao. Uhusiano utaendelea kuwa mzuri. Pia tunashukuru sana wananchi wa Zambia ambao wamekuwa wakituombea na kutuunga mkono katika kipindi hiki kigumu. Edgar Lungu aligusa mioyo ya watu wengi Zambia, na tunabaki kushukuru kwa upendo huo.”

Uamuzi huu sasa unafungua ukurasa mpya kwa familia kuendelea na mipango ya mazishi, huku ikitarajiwa kutoa taarifa zaidi kuhusu hatua zinazofuata na tarehe ya mazishi katika siku zijazo. Serikali ya Zambia nayo imesisitiza kuwa itaheshimu mchakato huo kama jambo la kifamilia.

Rais huyo wa zamani wa Zambia, alifariki mwaka jana akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo jijini Pretoria, na tangu wakati huo mwili wake ulikuwa bado haujafanyiwa mazishi rasmi kutokana na mvutano uliodumu kati ya familia na serikali kuhusu mahali pa kuzikwa kwake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW