Hatimaye mbinyo wazidi kwa Theresa May kuondoka madarakani
23 Mei 2019Hayo ni baada ya mpango wake wa hivi karibuni wa Brexit kukosolewa kwa kiasi kikubwa.
Mswada wa sheria ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya wa waziri mkuu Theresa May uliondolewa bila kutarajiwa kutoka katika mpango wa shughuli za serikali bungeni mapema mwezi Juni, leo Alhamis, na kuzusha tetesi zaidi kuhusu hali yake ya baadaye.
Serikali ya chama cha Conservative imekuwa ikitarajia kuweka msukumo katika mswada wa makubaliano ya kujitoa hapo kesho Ijumaa katika baraza la wawakilishi, la wabunge wa kuchaguliwa. Lakini Mark Spencer, akikaimu nafasi ya kiongozi wa bunge hilo kutoka chama cha May, Andrea Leadsom, ambaye alijiuzulu jana, amesema serikali sasa itachapisha mswada baada ya bunge kwenda mapumziko kuanzia Ijumaa hadi Juni 3.
Mbunge Mel Stride aliteuliwa kuwa kiongozi wa serikali bungeni katika baraza la wawakilishi leo, akichukua nafasi ya Andrea Leadsom ambaye amejiuzulu akipinga mkakati wa waziri mkuu May katika Brexit.
Shughuli za serikali bungeni
Stride ambaye, hapo kabla alikuwa naibu waziri katika wizara ya fedha, atachukua jukumu hilo la uwandamizi ambalo linabeba wajibu wa kuendesha shughuli za serikali bungeni.
Waziri mkuu May yumo katika mbinyo wa kutaka ajiuzulu baada ya juhudi zake za mwisho za Brexit kugonga mwamba na amekubali kukutana na mwenyekiti wa chama chake cha Conservative kesho Ijumaa kujadili juu ya hatma yake. Kuna idadi kadhaa ya viongozi wa chama cha Conservative ambao wako njiani kuwania wadhifa wa waziri mkuu May.
Boris Johnson ambaye alijiuzulu kuwa waziri wa mambo ya kigeni mwezi Julai kuhusiana na upinzani wake dhidi ya May alivyolishughulikia suala la majadiliano ya kujitoa nchi yake katika Umoja wa Ulaya ni mmoja kati ya wanaotarajiwa kuwania kiti cha Theresa May.
Mbunge wa bunge la Ulaya Guy Verhofstadt amesema leo kwamba kura ya maoni iliyopigwa Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa ulaya , ilikuwa ni maafa kwa Ulaya , lakini imekuwa na athari kwamba hakuna mtu mwingine katika bara hilo anataka kuona nchi nyingine ikijitoa kutoka Umoja huo.