1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye McCarthy achaguliwa spika nchini Marekani

7 Januari 2023

Mwanasiasa wa chama cha Republican Kevin McCarthy amechaguliwa kuwa spika mpya wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani baada ya duru 15 za uchaguzi kushindwa kumpa ushindi.

USA Sprecherwahl im Repräsentantenhaus l McCarthy zum neuen Sprecher gewählt
Kevin McCarthy wa Republican akiapishwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Ushindi wake unafuatia juhudi za siku kadhaa za kuwashawishi wanasiasa wenzake wa chama cha Republican ambao walikataa kumuunga mkono.

Uasi huo wa kisiasa ulisababisha mparaganyiko mjini Washington na kuzuia kuanza kwa shughuli za Baraza la Wawakilishi, chombo muhimu katika utawala wa Marekani.

"Baba yangu mara zote aliniambia, haijalishi vile ulivyoanza, bali vile ulivyofanikiwa kumaliza” alisema McCarthy muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa spika.

Wanasiasa wa chama chake walishangalia hotuba fupi iliyotolewa na mwanasiasa huyo.

Atoa ahadi ya kuudhibiti utawala wa Joe Biden 

McCarthy alitumia muda mwingi kuwashawishi wanasiasa wenzake kumuunga mkono.Picha: Andrew Harnik/AP/picture-alliance

Akionesha dhamira ya kuukabili utawala wa rais Joe Biden na chama cha Democratic, McCarthy ameahidi kufungua uchunguzi wa masuala chungunzima ya utawala wa Biden na kutumia nguvu za Bunge kusaka majibu.

"Hivi sasa kazi ngumu inaanza", alitanabahisha mwanasiasa huyo wa Republican kutoka California.

Alimshukuru rais wa zamani Donald Trump kwa kuwa naye bega kwa bega kwenye mchakato wa kusaka uspika, ikiwemo kupiga simu kadhaa "kutafuta kura za mwisho mwisho”.

Warepublican walishangilia kwa bashasha pale matokeo yalipotangazwa huku wakipaza sauti wakitamka maneno "Marekani, Marekani”.

Baada ya shamra shamra za muda mfupi, McCarthy aliapishwa rasmi kuwa spika na kisha akawaapisha wabunge wapya waliokuwa wakisubiri kwa wiki nzima.

Kuchaguliwa kwa McCarthy kumewezesha kufunguliwa rasmi kwa shughuli za Baraza la Wawakilishi kwa muhula wa mwaka 2023-24.

Ushindi uliopatikana kwa taabu unaweza kumponyoka 

Uchaguzi wa spika uligubikwa na songombingo ukumbini.Picha: Andrew Harnik/AP/picture-alliance

Ushindi wa McCarthy ulipatikana baada ya kufanikiwa kuwashawishi zaidi ya wajumbe 12 waliokuwa wakimpinga ikiwemo mwenyekiti wa kundi la wabunge wanaojiita wapigania Uhuru.

Katika duru ya 14 ya uchaguzi, McCarthy alikosa kura moja na kukazuka zogo kubwa kwenye ukumbi wa Bunge. Hata hivyo alifanikiwa kumshawishi mjumbe mmoja na katika duru ya 15 alipata idadi ya kura zilizohitajika kumwezesha kuwa Spika.

Hata hivyo ushindi wake haukuja mikono mitupu. Mwanasiasa huyo alilazimika kuridhia matakwa kadhaa ya wale waliokuwa wakimpinga. Miongoni mwa mambo aliyoridhia ni kubadili kanuni za Bunge kuruhusu hata mbunge mmoja tu kuleta hoja mezani ya kumwondoa madarakani.

Hilo linaamanisha ingawa McCarthy amepata ushindi, bado atakuwa spika asiye na uhakika wa nafasi yake ikitiliwa maanani uwezekano wa kuwekewa kigingi na wapinzani wake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW