Hatimaye Zuma ajisalimisha kwa polisi
8 Julai 2021Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amejisalimisha kwa polisi ili kuanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela.
Wakfu wa Zuma Foundation uliandika katika mtandao wake wa Twitter kuwa kiongozi huyo ameamua kuheshimu agizo la korti na kwamba alikuwa njiani kuelekea katika kituo cha polisi cha wilaya ya Kwa Zulu-Natal.
Msemaji wa polisi Lirandzu Themba amethibitisha kuwa Zuma yuko chini ya ulinzi wa polisi baada ya kujisalimisha.
Dakika chache tu kabla ya muda wa mwisho aliyopewa na korti kujisalimisha kwa hiari kabla ya polisi kumkamata, Zuma aliondoka nyumbani kwake Nkandla akisindikizwa na msafara wa magari.
Zuma ameamua kujisalimisha kwa mamlaka ili kutii agizo la mahakama ya katiba nchini humo iliyomkuta na hatia ya kudharau agizo la mahakama na kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela.