Hatma ya Super League mikononi mwa mahakama ya Ulaya
13 Mei 2021Mahakama mjini Madrid imeiomba mahakama ya haki ya Ulaya kuamua ikiwa FIFA na UEFA zinakiuka sheria za ushindani za Umoja wa Ulaya kwa kuzizuia klabu kuandaa mashindano ya Ulaya ya Super League.
Mahakama hiyo pia inaitaka mahakama ya haki kuamua kama FIFA na UEFA wanaweza kuzifungia au kuziadhibu klabu ambazo bado zimesalia katika mchakato wa mashindano hayo.
Mashindano ya Super League yalitangazwa mwezi uliopita na klabu 12 waanzilishi lakini yalivunjika chini ya saa 48 baada ya tangazo kufuatia ghadhabu kutoka kwa mashabiki, serikali, wachezaji na makocha.
Klabu 8 za Manchester United, Liverpool, Manchester City, Chelsea, Tottenham Hotspur, Arsenal, AC Milan, Inter Milan na Atletico Madrid zilijiondoa na kukubali kuadhibiwa na UEFA kwasababu ya kuwa sehemu ya mchakato. Hata hivyo Real Madrid, Barcelona na Juventus ambazo ni miongoni mwa timu waanzilishi hazijajitoa michuano hiyo.
UEFA ilitangaza Jumatano kuteua wachunguzi wa kinidhamu kufanya uchunguzi ikiwa klabu hizo tatu zimekiuka mfumo wa sheria wa shirikisho hilo.