Hatma ya Ugiriki katika Umoja wa Ulaya inatiliwa shaka
18 Juni 2015Huku mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha duniani IMF yakigonga mwamba wiki hii, maafisa wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wameanza kujadili wazi uwezekano wa Ugiriki kuondoka kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro.
Hapo jana, siku moja kabla ya mkutano wa nchi wanachama 19 wa kanda hiyo inayotumia sarafu ya euro kufanyika, benki kuu ya Ugiriki kwa mara ya kwanza ilionya kuwa nchi hiyo huenda ikalazimika kujiondoa kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro na hata kutoka kwa Umoja wa Ulaya iwapo itashindwa kufikia makubaliano na wakopeshaji wake.
Benki hiyo imesema kuondoka kwa Ugiriki katika kanda inayotumia sarafu ya euro kutasababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi, kupungua pakubwa kwa mishahara na kuongezeka maradufu kwa ukosefu wa ajira katika taifa hilo la kusini mwa Ulaya.
Kuondoka kwa Ugirki kwajadiliwa wazi
Na kama ishara ya kuwa uwezekano huo wa kujiondoa kwa Ugiriki katika umoja huo ni jambo ambalo linazingatiwa, mkuu wa benki kuu ya Ujerumani Jens Weidmann amesema kujiondoa kwa Ugiriki kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro kutabadili mkondo wa uthabiti wa sarafu hiyo lakini haitaiporomosha kwani kanda hiyo haiitegemei Ugiriki.
Licha ya onyo hilo la kuondoka kwa Ugiriki na nchi hiyo kutarajiwa kuilipa IMF euro bilioni 1.6 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu,waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amesema hatarajii mzozo wa kuitaka Ugiriki kufanya mageuzi magumu ya kiuchumi ili ipewe mkopo zaidi wa uokozi kutatuliwa katika mazungumzo ya leo na kuongeza ni viongozi wa kisiasa ndiyo wanaoweza kufikia makubaliano hayo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana imani kuwa makubaliano na Ugiriki yanaweza kufikiwa kwani palipo na nia pana njia na kuongeza angeitaka nchi hiyo kusalia katika kanda inayotumia sarafu ya euro.
Marekani pia yatiwa wasiwasi
Mgogoro huo wa kiuchumi umeitia wasiwasi pia Marekani. Mkuu wa benki kuu ya Marekani Janet Yellen ameonya uchumi wa dunia utakumbwa na msukosuko iwapo Ugiriki na wakopeshaji wake watashindwa kufikiana.
Yellen amesema kukosa makubaliano muhimu ya kiuchumi anaona kutakuwa na matatizo yatakayoikumba Ulaya na masoko ya fedha duniani
Kura za maoni zinaonyesha wengi wa wagiriki wanaunga mkono mkakati unaotumika na serikali katika kufanya mazungumzo na wakopeshaji wake. Kiasi ya watu 7,000 waliandamana hapo jana jioni katika mji mkuu wa Ugiriki Athens, kupinga masharti ya wakopeshaji ya kutaka serikali ibane zaidi matumizi.
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras anatarajiwa kuhudhuria hii leo jukwaa la kiuchumi la kimataifa nchini Urusi na kufanya mazungumzo hapo kesho na Rais wa Urusi Vladimir Putin hatua ambayo wachambuzi wanasema ni ishara kuwa Tsipras anajaribu kuuonyesha umoja wa Ulaya kuwa ana mikakati mingine ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi unaoikumba nchi yake.
Mwandishi: Caro Robi/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga