Uteuzi wa Muhoozi kuwa CDF wa Uganda wazua hisia mseto
22 Machi 2024Ni rasmi kuwa mwanawe rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba sasa ndiye ana mamlaka ya juu zaidi juu ya masuala ya usalama na ulinzi wa ndani na nje ya nchi.
Mamlaka ya mkuu wa majeshi yalifanyiwa mageuzi na kutangazwa mwezi uliopita wa Februari. Kwa baadhi ya wadadisi na wanasiasa, uteuzi wa Jenerali Muhoozi kuwa mkuu wa majeshi ulipangwa tangu zamani.
Kwa hiyo si ajabu kwamba sasa umehalisika katika kipindi kuelekea msimu wa uchaguzi mkuu. Kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye amesema kwamba "nchi hii ilikwisha tekwa serikali sasa imetekwa kwani hata majeshi yametekwa na familia".
Kwa upande mwingine, kuna mtazamo kuwa sasa Museveni amemdhibiti vilivyo mwanawe ambaye alikuwa ametangaza kugombea urais na kuzindua vuguvugu la kumpigia debe.
Wiki iliyopita vuguvugu hilo lijulikanalo kama PLU liliendesha mkutano wa hadhara mojawapo ya ngome kuu za upinzani mjini Masaka na kuvutia umati mkubwa wa watu.
Soma: Rais Museveni amteuwa mwanawe kama mkuu wa jeshi la ulinzi la Uganda
Hali hii imesababisha mashaka hasa katika chama kikuu cha upinzani NUP ambacho rais wake Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine kwa sasa yumo katika mvutano na mwanasiasa mkuu wa sehemu hiyo Matthias Mpuga.
Lakini zaidi ni kwamba, Muhoozialidhihirisha kuwa anaweza kuleta vishindo katika uchaguzi mkuu akigombea urais. Katika mabadiliko aliyofanya rais Museveni kwenye baraza lake la mawaziri, baadhi ya wafuasi wakuu wa Muhoozi wamepewa nafasi za uwaziri. Mwanahabari na mdadisi wa maswala ya kisiasa John Kibego ametoa mtazamo huu.Museveni amuondoa mwanae ukuu wa jeshi, ampandisha cheo
"Museveni amejiweka katika nafasi ambapo ikiwa hataweza kuendelea kuongoza nchi ataweza kukabidhi mamlaka kwa mwanawe kwa njia rahisi, watu wamekuwa wakimtaja Muhoozi kuwa mtambo wa jenereta unaosubiri kuashwa sasa tunaweza kusema umeashwa".
Kulingana na katiba ya nchi, mwanajeshi haruhusiwi kujihusisha katika masuala ya kisiasa. Hii ina maana kuwa akiwa kwenye wadhifa wa juu zaidi katika jeshi, Jenerali Muhoozi atatarajiwa kuondokana na harakati zake za kuwa rais. Watu mbalimbali wametoa maoni haya. "Bila shaka Museveni sasa ametuweza, haweza kung'atuka ila kwa hiari yake na ana uhakika bado atakuwa na mamlaka kwa taifa”. "Huu ni dikteka wa kiwango cha juu, mke ni waziri wa elimu akithibiti hali ya elimu na taasisi zote za elimu. Sasa mtoto ndiye anasimamia majeshi yote na vyombo vya dola ikiwemo polisi na magereza”
Fuatilia: Muhoozi atangaza azma ya kuchukua urais wa Uganda
Miongoni mwa wale ambao wamepoteza nafasi zao ya uwaziri ni wale waliodaiwa kuhusika katika wizi wa mabati yaliyokusudiwa kwa jamii za Karamoja.