1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya rais Samia kuhimiza uvaaji barakoa wazusha gumzo

Hawa Bihoga11 Mei 2021

Mwenendo wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuonekana kuhimiza matumizi ya barakoa katika hafla za kimataifa kumezua mseto wa majadiliano miongoni mwa Watanzania.

Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Wengine wasema ni sehemu ya kuliandaa taifa hilo kuingia kwenye hatua za kuzuia maambukizi licha ya kwamba halijatangaza hali ya maradhi hayo tangu mwaka uliopita

Mwenendo wake wa uvaaji wa barakoa umeonekana kushika kasi zaidi tangu aliporejea nchini baada ya kutembelea mataifa jirani ya Kenya na uganda ambayo yamekuwa yakitoa muelekeo wa mataifa yao juu ya hali ya virusi vya corona kila hatua, hata kufikia katika hatua ya kutoa chanjo.

Kulingana na Rais Samia mwenyewe alipokutana na wazee jijini Dar es salaam alisisitiza utamaduni wa barakoa katika mazungumzo yao ulilenga kulikinga kundi hilo dhidi ya hatari mbalimbali ikiwemo janga la corona.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Uganda 11.04.2021Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Mwenendo huu umezua mawazo mseto miongoni mwa wananchi, wakihoji je hiyo ni sehemu ya kuliandaa taifa kuanza kutekeleza miongozo ya shirika la afya ulimwenguni dhidi ya maambukizi ya corona ukizingatia mtangulizi wake aliweka wazi kuwa taifa hilo la afrika mashariki lipo huru dhidi ya maradhi hayo?

Itakumbukwa kuwa Rais Samia anatekeleza hayo wakati taifa likisubiri matokeo ya kamati alioiunda ili kufuatilia mwenendo wa maradhi hayo ulimwenguni ili ipate kuishauri serikali juu ya hatua za kuchukua ikiwa ni sehemu ya kuungana na dunia kumaliza maradhi hayo ambayo yamekwisha gharimu maisha ya watu zaidi ya milioni tatu na kuyumbisha uchumi ulimwenguni kote.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaona, mwenendo huu wa Rais Samia unaanza kuakisi yale ambayo yatapendekezwa na kamati alioiunda na hivyo ni sehemu ya kuliandaa taifa kisaikolojia kutilia mkazo miongozo ya kimataifa.

Rais Samia Suluhu Hassan akikutana na mwenyeji wake rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika ikulu ya rais jijini Nairobi Mei 4, 2021.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya virusi vya corona Tanzania imetoa kwa wakaazi nchini humo miongozo 15, ikiainisha tahadhari za kuchukua ili kujikinga na maambukizi ikiwemo uvaaji wa barakoa, kuhimiza kunawa mikono na matumizi ya tiba mbadala ikiwemo kijifukiza.

Tanzania pekee katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na jumuia ya maendeleo kusini mwa afrika SADC bado haijakubaliana na baadhi ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na janga la corona, ikiwemo suala la chanjo, ambapo sasa masikio yanaelekezwa kwenye kamati je suala hilo litachukuliwa kwa ukubwa gani?