1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Hatua ya Samia kuhusu Covid ni ya kupongeza

28 Julai 2021

Hatua ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusu kukabiliana na janga la virusi vya Corona kinyume na mtangulizi wake John Magufuli, inatia matumaini na inapaswa kuungwa mkono, anaandika Lillian Mtono katika uhariri.

Tansania | Amtseinführung Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP Photo/picture alliance

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anasubiri ripoti ya timu ya wataalamu aliyoiunda kumshauri hatua za kuchukuwa kukabiliana na janga la virusi vya corona, huku tayari akiwaomba raia kuchukuwa hadhari kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 aliosema upo nchini mwake, kinyume kabisa na msimamo wa mtangulizi wake Marehemu John Magufuli ambaye wengi wanasema aliishi katika hali ya kuukana. Je, hatua za sasa za Rais Samia zinatosha na hazijachelewa? Lilian Mtono na Maoni yafuatayo.

Akizungumza na viongozi wa dini waliokusanyika jijini Dodoma kwa lengo la kumuenzi Marehemu Magufuli na kuiombea nchi siku  ya Jumapili (Aprili 18), Rais Samia alibainisha kuwa tume aliyoiunda wiki chache nyuma ilikuwa karibuni kumaliza kazi zake na kwamba baada ya kupokea ripoti na ushauri wao ataijulisha nchi kitu cha kufanya.

Wakati akitangaza kuunda tume hiyo, Rais Samia alisema, Tanzania sio kisiwa na ni lazima ifike mahala ikubali kuungana na jumuiya ya kimataifa katika mapambano hayo.

Mwandishi wa DW Kiswahili Lillian Mtono.Picha: DW/L. Richardson

Si mtazamo mpya kwa Tanzania. Wakati wa wimbi la mwanzo mwaka jana, serikali ya Magufuli ilianza kuchukuwa hatua kadhaa za kiafya kama zilivyoagizwa na wataalamu wa afya na Shirika la Afya Duniani (WHO). Kuliwekwa itifaki ile ile ya kilimwengu: kukusanya data, kufanya vipimo, kufuatilia mkufu wa waliokutana na mtu aliyeambukizwa, kuwatenga walioambukizwa na pamoja na uvaaji barakowa, matumizi ya vitakasa mikono na kuweka masafa.

Lakini hayo yalidumu kwa mwezi mmoja tu. Ghafla, Marehemu Rais Magufuli ambaye kitaaluma alikuwa mwanasayansi, akaanza kutilia shaka virusi vyenyewe, akikosowa ukweli wa vipimo na akageukia kwenye sala na maombi, huku akitilia mkazo watu kutumia tiba za asili, maarufu kama nyungu. Baada ya tangazo siku tatu za maombi, Tanzania ya Magufuli unasahau kabisa kuhusiana na janga hilo. Watu wakatupa barakoa na kuacha kila hatua ya kujikinga na maisha yakaendelea.

Takwimu za mwisho za wagonjwa wa COVID-19 zilizotolewa na serikali katikati ya mwaka jana zilionyesha Tanzania ilikuwa na wagonjwa 509 na tangu hapo hakukutolewa takwimu nyingine, hata baada ya miito kutoka WHO.

Lakini hadi kifo chake hayati Magufuli hakuwahi kukiri hadharani kwamba kuna kitisho cha maambukizi nchini humo. Hata baada ya taarifa za kuongezeka kwa vifo na miito kwa serikali ya kuitaka kutamka wazi bado serikali iliziba masikio na kusema kinachosababisha vifo ni "changamoto ya kupumua.”

Lakini cha kushangaza kulianza kuonekana hatua kadhaa kuchukuliwa. Kwa mfano kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili kulizinduliwa huduma ya tiba ya kujifukiza na serikali ikawaalika watanzania kupata huduma hiyo. Hawakusita, wakajazana tele. Hatua hii ilichagizwa na matamshi ya rais hayati Magufuli kwamba wapo watanzania waliokwenda nje, wakachoma chanjo wakarudi Tanzania na corona ya ajabu ajabu.

Mtangulizi wa Samia, John Magufuli alikuwa mpinzani mkali wa chanjo na alitilia mashaka hatari ya uganjwa wa Covid-19.Picha: Luke Dray/Getty Images

Ingawa wataalamu wa shirika la afya duniani WHO walisema tiba hiyo ni hatari na inaweza kusababisha maji kujaa kwenye mapafu. Lakini walikuwa  wamechelewa, kwa sababu hiyo ilikuwa ni awamu ya tatu ya kupiga nyungu.

Na hata baada ya kifo chake kulitarajiwa labda mambo yangebadilika, lakini haikuwa hivyo, ingawa machache yameonekana tangu baada ya kifo cha Magufuli. Baadhi walionekana kama wamekurupushwa usingizini na kuanza kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko bila ya woga. Hata baadhi ya viongozi wa serikali ambao hawakuwahi kuthubutu hapo kabla, walivaa!

Bado si rahisi hata sasa kuwaaminisha baadhi ya watanzania kwamba corona ingalipo na wanatakiwa kujilinda. Kwa mfano, ripoti ya hivi majuzi ya Kituo cha Kukabiliana na Maradhi barani Afrika (CDC) iliposema imegunduwa aina mpya ya kirusi cha corona kinachojibadilisha maumbile kwa msafiri aliyekuwa akitokea Tanzania kuelekea Angola na ambacho kiliweza kujibadilisha umbo lake karibu mara 40, taarifa ilipochapishwa kwenye kurasa za DW Kiswahili za mitandao ya kijamii, maoni ya wengi kutoka Tanzania yalijaa kebehi, matusi na tuhuma za kila aina. Wengi wakisema, "DW msitulazimishe kuwa Tanzania ina corona!” 

Uhamaishaji wa watu kujilinda dhidi ya Covid-19.Picha: Eric Boniphace/DW

Hii inaashiria kwamba Watanzania  wengi bado wanaona kama hawahusiki kabisa na janga hili na wanalichukulia kirahisi sana, tena hawataki kujisumbua nalo. Wengine ndio tayari walikwishaaminishwa kwamba janga hilo halipo baada ya kuambiwa na viongozi wa serikali, na hawa hawabadiliki kirahisi, lakini wengine ni wale wanaofuata upepo tu, wanasema liwalo na liwe.

Ni mwaka jana tu ambapo Tanzania iliruhusu mamia kwa maelfu ya watalii kuingia nchini humo, huku ikijisifu kwamba wanakuja nchini humo kwa sababu wanaamini Tanzania iko salama. Lakini ni kwa kiasi gani ilijihami dhidi ya maambukizi kutoka nje? Je watalii walishurutishwa kuvaa barakoa ama kukaa karantini kwanza? Je, walipimwa kwanza ili kujua iwapo walikuwa na maambukizi ama la. Udhibiti ulikuwaje?

Kwa hivyo, Rais Samia, ninachoweza kusema hapa ni kwamba ili kuondoa sintofahamu iliyopo ni lazima utamke jambo. Watu wengi wanaisubiri mamlaka iseme. Na huo ni uwajibikaji wa serikali mbele ya raia wake. Kuhakikisha usalama wa afya zao.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW