1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya Tanzania kuwaondoa Wamasai yazidi kuibua hisia

Admin.WagnerD13 Juni 2022

Hatua ya serikali ya Tanzania ya kuziondoa jamii za wamasai kwenye eneo lenye mzozo la Loliondo kaskazini mwa nchi hiyo linaendelea kuibua hisia kali hata katika taifa jirani la Kenya.

Afrika Tansania Protest Maasai
Picha: DW

Baadhi ya viongozi wa Narok nchini Kenya wamelaani vikali madai ya kujeruhiwa na kujaribu kutimuliwa kwa nguvu Wamaasai hao kutoka eneo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Uokozi na Taasisi ya Oakland, hali ya wasiwasi iliibuka Jumatano baada ya polisi kuongoza juhudi za kuwaondoa Wamaasai kwa nguvu. Kumekuwa na picha kwenye mitandao na video zikionesha jinsi watu walivyojeruhiwa kwa risasi kwenye kisa hicho ambacho kimeibua malalamiko nje ya mipaka ya Tanzania.

Mbunge wa Narok Kaskazini nchini Kenya Moitalel Ole Kenta amedai hayo yanafanyika kwasababu serikali ya Tanzania imetoa leseni ya kuwinda kwa kampuni binafasi ya Ortello kutoka Falme za Kiarabu.

"Inasikitisha sana kuwa jamii ambayo imekuwa ikilinda hifadhi ya wanyamapori kwa karne nyingi sasa inaadhibiwa. Natoa wito kwa jamii ya Kimataifa kuingilia kati na kutafuta suluhisho." Alisema.

Hata hivyo serikali ya Tanzania imekanusha madai ya kutimuliwa  kwa Wamaasai kwa fujo, ikisema kuwa hakuna mtu yeyote aliyeondolewa kwenye hifadhi hiyo. Tanzania ilikuwa inalenga kuwaondoa wakazi kwenye hifadhi hiyo kwa lengo la kubadilisha hadhi yake na kuwa hifadhi ya wanyamapori.

Soma Zaidi: Tanzania yatuhumiwa kuzuia huduma za jamii Ngorongoro

Wanyama aina ya Pundamilia kama wanavyoonekana kwenye mbuga za Ngorongoro.Picha: J. Sorges

Mwaka 2021, Rais Samia Suluhu alisema kuwa mipango ya kuwaondoa watu kwenye hifadhi hiyo ilitokana na kuongezeka kwa idadi yao hivyo kubinya ongezeko la wanyamapori. Lydia Ntimama ni mwaniaji wa kiti cha uwakilishi wa kike katika jimbo la Narok.

Alilalama "Ule uchungu tunahisi, watoto wetu wanapigwa risasi, vijana wetu wanapigwa risasi, wazee wetu wanaumia, rais Suluhu, ile roho ya mama, tulifurahi sana tuliposikia mama amechaguliwa, ni uchungu sana tukiona mama anaumiza watu. Kama mama uchungu ni mwingi.”

Serikali ya Tanzania ilikuwa inapanga kuwahamisha wenyeji hao kwenye shamba la ekari 162,000 lililoko katika wilaya ya Handeni. Wakili Martin Ole Kamwaro ametoa hakikisho kuwa watazingatia taratibu za kisheria kwa watu walioathiriwa.

"Naiambia dunia watuchunge kama watu wa asili, maana hii ni ukoloni mambo leo na wanataka kurejesha, na wakati huu hatutakubali kama Wamaasai wa Kenya na Tanzania.”  Alisema Kamwaro.

Mwaka 2018, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, iliagiza Tanzania kutowatimua Wamaasai ama kuwadhulumu watu waliokuwa wanaishi karibu na hifadhi hiyo ambayo ni turathi ya ulimwengu. 

Baadhi ya wamasai Tanzania waandamana kupinga kuondoshwa eneo la hifadhi

02:19

This browser does not support the video element.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW