1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua za Kinga dhidi ya Udukuzi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
8 Januari 2019

Hatua za kinga dhidi ya udukuzi, Robert Habeck kuacha kuitumia mitandao ya kijamii na mjadala kama Olaf Scholz agombea kiti cha kansela kwa tikiti ya chama cha SPD uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwaka 2012 magazetini.

Deutschland Bundesamt für Sicherheit in der Informationstechnik (BSI)
Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

 

Tunaanza na hatua za kuhakikisha data ziko salama mitandaoni. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika: "Kashfa ya kudukuliwa data zisizokuwa na idadi inawasumbuwa safari hii wanasiasa, wasanii na watu wengine mashuhuri. Hata hivyo isisahauliwe kwamba zamani  data za mamilioni ya wanaotumia mitandao mfano wa Facebook zimekuwa zikidukuliwa. Hujuma kama hizo zinaweza kumuathiri yeyote yule. Kadhia kama hizo hazishi kuripotiwa lakini sio wengi wanaoshughulika kusaka njia ya kuzikinga data zake."

Ushirikiano na juhudi kuunganishwa ili kuleta tija

Gazeti la Weser-Kurier linahoji urasimu ndio wa kulaumiwa. Gazeti linaendelea kuandika: "Mfumo wa kinga dhidi ya udukuzi nchini Ujerumani mara nyingi unashindwa kufua dafu mbele ya wadukuzi. Chanzo cha hali hiyo kinatokana na vurugu katika idara zinazohusika na usalama na kinga mitandaoni. Idara hizo ni pamoja na idara ya serikali kuu inayoshughulikia masuala ya usalama na teknolojia ya habari, kituo cha kinga dhidi ya udukuzi (BSI)  kituo kikuu cha teknolojia ya habari na usalama (ZITIS), ofisi ya mwendesha mashitaka inayoshughulikia masuala ya udukuzi mjini Frankfurt, idara maalum za polisi, idara za upelelezi na jeshi la shirikisho-Bundeswehr. Na zaidi ya hayo kila jimbo lina mipango yake wenyewe ya kukabiliana na kitisho hicho. Wakati umewadia sasa wa kuunganisha juhudi zote hizo."

Habeck akirejeshea nuru yake chama cha die Grüne

Kiongozi mwenza wa walinzi wa mazingira die Grüne, Robert Habeck ametangaza azma ya kutotegema sana mitandao ya kijamii. Uamuzi huo umepokelewa kwa maoni tofauti na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Katika wakati ambapo baadhi wanamkosoa, wengine wanasifu uamuzi wake. Gazeti la "Badische-Zeitung" linaandika: "Robert Habeck anatajwa kuwa kabahatika kisiasa. Kwa ushirikiano pamoja na kiongozi mwenzake Annalena Baerbock, anasifiwa kuwa sababu ya kunawiri upya chama cha walinzi wa mazingira die Grüne na kuambatana na wakati. Kuna uwezekano mkubwa kuona uamuzi wake wa kuachana na mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook ukizidi kukipatia sifa chama hicho na kugeuka chama cha mapambazuko ya kisiasa."

Ndoto ya waziri wa fedha Olaf Scholz kuwa kansela

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu mjadala uliosababishwa na tamko la waziri wa fedha wa serikali kuu Olaf Scholz kwamba atagombea kiti cha kansela uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwaka 2021. Gazeti la Leipziger Volkszeitung linaandika: "Anaonekana kana kwamba anaota na hatambui kwamba hakuna, si wapiga kura wanaotaka kuwa na kansela wa chama cha SPD na wala si chama chake cha SPD kinachomtaka awe mgombea wao. Hata kama Scholz anaweza kuwa kansela mzuri lakini haitoshi, anabidi pia awe na uwezo wa kufanikiwa kuipanda ngazi hiyo. Na kwa mujibu wa hali ya mambo, Scholz sio tu hatokuwa kansela bali hatoachiwa pia kugombea wadhifa huo."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilheir/Inlandspresse

Mhariri: Caro Robi