1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hayati John Joseph Pombe Magufuli aagwa mjini Dodoma

22 Machi 2021

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaongoza viongozi kutoka sehemu mbalimbali duniani na Watanzania kwa ujumla kumuaga aliyekuwa rais wa nchi hiyo, hayati John Pombe Magufuli, alifariki dunia tarehe 17 mwezi Machi

Tansania | Beisetzung Präsident John Magufuli in Dar es Salaam
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Akihutubia wakati wa shughuli ya kitaifa kuaga mwili wa Magufuli kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma,  Rais Samia ametoa hofu wenye mashaka kuhusu uongozi wake akisema yuko tayari na anao uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa. 

Rais Samia amesema licha ya yeye kuwa ni mwanamke, yuko imara na kwamba amepita kwenye mikono ya hayati Magufuli na hivyo amejifunza mengi kwa sababu alikuwa sio mtu wa kuyumbishwa na mwenye msimamo thabiti kwa kile alichoamini kina maslahi kwa Watanzania na kwamba yeye ataliongoza taifa bila mashaka yoyote. 

"Kwa wale ambao wana mashaka mwanamke huyu ataweza kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwambie huyu aliyesimama hapa ni rais, wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni  mwanamke," alisema Rais Samia Suluhus Hassan

Aidha amesema yeye pamoja na viongozi wenzake wako tayari kuiendeleza miradi yote iliyoanzishwa na serikali chini ya uongozi wa Magufuli.

Maraisi waliohudhuria wasema wako tayari kufanya kazi na Rais Samia Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: AP Photo/picture alliance

Shughuli hiyo ya kitaifa kwa ajili ya kuuaga mwili wa hayati Rais Magufuli imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ambao walimuelezea kiongozi huyo kuwa Simba wa Afrika kutokana na uchapakazi wake na namna alivyoitetea Tanzania pamoja na bara la Afrika. 

Wakitoa salaam zao za rambirambi Rais wa Kenya Uhuru Kenyata, Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe wamesema Tanzania, Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika, SADC na bara zima la Afrika, wamepoteza mtu muhimu. 

Maelfu ya watu wamejitokeza kumuaga hayati Magufuli huku kukizuiwa watu kuingia uwanjani kutokana umati uliofurika ili kuweza kuondoa hatari ya kutokea majanga ya watu kujeruhiwa kutokana na kukanyagana.

Mwandishi: Deo Kaji Makomba.