Hazina: Deni la Kenya lapanda hadi kiwango cha kihistoria
16 Agosti 2023Jumla ya deni la umma lilipanda kwa rekodi ya shilingi trilioni 1.56, sawa na dola bilioni 10.8, katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 hadi shilingi trilioni 10.1, sawa na dola bilioni 70.75, na kuvuka ukomo wa deni wa shilingi trilioni 10, kulingana na data iliyotolewa Jumanne.
"Ongezeko la deni la umma limechangiwa na utoaji wa mikopo ya nje, kushuka kwa kiwango cha ubadilishaji fedha na kulipwa kwa deni la ndani na nje,” hazina ilisema.
Gharama za marejesho ya mikopo, hasa kwa China, zimeongezeka huku sarafu ya nchi hiyo ikibadilishwa kwa kiwango cha chini kabisa cha takriban shilingi 144 kwa dola.
Soma pia: Umoja wa Ulaya na Kenya zafikia makubaliano ya kibiashara
Gharama ya kulipa deni katika mwaka ulioishia Juni ilikuwa shilingi bilioni 391, sawa na dola bilioni 2.7, ambapo malipo ya juu zaidi -- shilingi bilioni 107, sawa na dola milioni 743 -- yalikwenda China.
Ukubwa wa deni umesababisha maonyo kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya kukadiria mikopo ikiwa ni pamoja na Fitch Ratings ambayo mwezi uliopita ilishusha uwezo wa Kenya wa kulipa wakopeshaji wa kimataifa kutoka "imara hadi hasi", ikitaja ongezeko la ushuru na machafuko ya kijamii.
Wabunge wa Kenya walipiga kura mwezi Juni kubadilisha kiwango cha ukomo wa deni kutoka kiasi cha shilingi kilichopangwa hadi sehemu ya pato la taifa (GDP). Seneti bado haijapitisha marekebisho hayo.
Ahadi ya Ruto kupunguza deni la serikali
Ruto aliingia madarakani mwaka jana kwa ahadi ya kufufua uchumi katika nchi hiyo yenye takriban watu milioni 53.
Ukuaji wa uchumi ulipungua hadi asilimia 4.8 mwaka 2022 kutoka asilimia 7.6 mwaka uliopita na unatabiriwa kuongezeka kwa zaidi ya asilimia tano mwaka huu, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Soma pia:Bei ya mafuta yapanda maradufu nchini Kenya
Akielezea mpango wake wa mageuzi ya kiuchumi kuanzia "chini juu", Ruto aliahidi kupunguza deni la serikali na kuanzisha sera za kutia pesa mifukoni mwa Wakenya maskini.
Lakini kitendo chake cha kwanza baada ya kushika wadhifa huo Septemba mwaka jana ilikuwa kupunguza ruzuku ya chakula na mafuta iliyoanzishwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, akisema alipendelea kutoa ruzuku kwa uzalishaji badala ya matumizi.
Mnamo Juni, Ruto alianzisha ushuru mpya ulioongeza bei ya bidhaa za msingi kama vile mafuta na chakula na uhamishaji wa pesa kwa simu, pamoja na ushuru wenye utata kwa walipa kodi wote kufadhili mpango wa nyumba.
Lakini katika mabadiliko ya msimamo siku ya Jumatatu, utawala wake ulirejesha sehemu ya ruzuku ya mafuta kufuatia duru kadhaa za maandamano ya vurugu dhidi ya serikali na hasira ya umma juu ya gharama kubwa ya maisha.
Ruzuku "ili kuwasaidia watumiaji kumudu ongezeko la bei za pampu" itaendelea kwa mwezi mmoja, mamlaka ya udhibiti wa nishati nchini ilisema.
"Matarajio ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kimataifa na uwezekano wa kudhoofika zaidi wa shilingi kutaitia majaribu dhamira ya serikali ya kudhibiti bei ya mafuta katika miezi ijayo," taasisi ya ushauri ya Oxford Economics Africa ilisema Jumanne, ikiongeza kuwa ruzuku hiyo ni kinyume na matakwa ya IMF.
Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi imara Afrika Mashariki lakini takriban theluthi moja ya wananchi wake wanaishi katika umaskini.
Mfumuko wa bei nchini Kenya umesalia kuwa juu, kwa kiwango cha kila mwaka cha asilimia 7.3 mwezi uliopita.
Ruto amesisitiza nyongeza ya ushuru inahitajika ili kuunda nafasi za kazi na kujaza hazina ya serikali na kupunguza utegemezi zaidi wa kukopa.