Hedhi salama bado ni changamoto kwa wasichana wa Kenya
27 Mei 2021Kupata hedhi ya heshima, mwanamke anahitaji, vitambaa vya hedhi ima vya kutumika mara moja au zaidi ya mara moja vikiwepo vya aina mbali mbali huku sabuni, maji na nguo ya ndani vikihusika kumhakikishia mwanamke usafi wa mwili wake.
Hata hivyo, kando na mtoto wa kike ambao wengi ni wanafunzi vile vile, mwanamke ambaye anajitafutia mtaji wa kila siku vitu hivi vingali changamoto kwake kupata huku pakikosekana maeneo ambayo ni safi na salama kwa wakati mmoja kuwasaidia angalau kujificha kuvaa au hata kubadilisha kitambaa cha hedhi wanapokuwa katika siku zai.
Carolyne Ojenge Ogot ambaye anajishugulisha na maswala ya wanawake katika nyanja na mashirika mbali mbali ikiwemo shirika la Linda Kesho - Kisumu katika wadhifa wa mshirikishi na pia shirika la Shiners Centre linalojihusisha na maswala ya wanawake na watoto anasema licha ya kuainishwa katika haki za kiafya na za kimsingi za kila mmoja kuhusu maslahi muhimu sawia na ilivyoainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu namba 6 yanayofafanua umuhimu wa makundi haya kushugulikiwa bado hayajaafikiwa kikamilifu bajeti ya matumizi ikiwa finyu.
"Wanawake bado wanateseka, wasichana wangali na mahitaji siku yao unapata hawaendi shule au akina mama hawawezu kuenda soko wala kutafuta maji ."
Anasema licha ya mpango wa serikali kutoa sodo kwa wasichana wa shule, mpango huu bado haujafaulu kuwafikia wote na ni wazi kuwa kulingana na takwimu kutoka wizara ya elimu nchini Kenya ikionyesha kuwa mtoto wa kike ambaye hukosa shule kwa siku nne kati ya siku 28 hii ikiwa na maana ya mwezi mzima hupoteza siku 13 za kusoma sawia na wiki 2 katika kila muhula wa masomo, sawia na siku 39 katika kipindi cha wiki 6 za masomo hii ikiwa ni hadi jumla ya miezi 9 katika kipindi cha masomo yake.o hupoteza miezi 9 za masomo.
'Serikali imetoa sodo kwa wasichana wanaoenda shule lakini haiwafikii."
Afisa wa maswala ya mipango kitengo cha afya ya uzazi ya vijana na wanawake katika shirika la vijana la Tiyo - Arthur Onyang'o anasema sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku ya Hedhi ya Heshima duniani, ni muhimu kwa serikali kuu na za kaunti kuekeza zaidi katika mafanikio ya lengo la hedhi ya hadhi miongoni mwa watoto wa kike na wasichana.
Kadhalika, amesema, mapungufu yaliyopo ni mengi na pana haja ya majukwa mbali mbali kuyazungumzia wazi wazi ili kuondoa unyanyapaa unaoweza kuandamana na minong'ono ya kijamii huku asilimia takriban 65 ya wanawake wakiwa hawana uwezo wa kumudu gharama ya kununua sodo.
"Watu wengi wanalichukulia jambo la hedhi kuwa swala la siri ."
Nchini Kenya, takwimu za wizara ya elimu bado zinaonyesha kuwa, mwanafunzi katika shule ya msingi wa kati ya darasa la 6 hadi 9 hupoteza majuma 18 ya kutosoma kati ya jumla ya wiki 108 za kalenda ya masomo na katika muda wa miaka minne ya shule za upili, mwanafunzi wa kike hupoteza siku 156 za kutosoma sawia na wiki 24 kati ya jumla ya wiki 144 zilizopo kwenye kalenda ya masomo.