1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heiko Maas anaelekea Uturuki na Ugiriki kutuliza mvutano

Sylvia Mwehozi
25 Agosti 2020

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas anaelekea Ugiriki na Uturuki katika juhudi za kutatua mvutano baina ya mataifa hayo mawili jirani, yanayosuguana juu ya haki za uchimbaji gesi bahari ya Mediterenia. 

Deutschland Heiko Maas reist nach Kiew
Picha: Imago Images/photothek/F. Gaertner

Ziara ya Maas inafanyika wakati Ugiriki ikianza mazoezi ya kijeshi yanayohusisha jeshi la wanamaji na lile la wana anga kwenye eneo ambalo Uturuki imetuma meli yake ya Oruc Reis iliyoambatana na meli za kivita, kwa ajili ya kufanya utafiti wa uwezekano wa hazina ya gesi na mafuta.

Katika kuijibu hatua ya operesheni za meli ya Uturuki, Ugiriki iliyaweka katika tahadhari majeshi yake na kutuma meli za kivita kufuatilia shughuli za Uturuki. Kabla ya kuzitembelea nchi hizo mbili, Maas aliwaeleza waandishi wa habari kwamba "Uturuki na Ugiriki ni washirika wetu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kwamba mzozo kwenye eneo la mashariki mwa Mediterenia unaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo ya dhati kwa kuzingatia sheria za kimataifa".

Meli ya Uturuki inayoendesha shughuli za utafiti mashariki mwa MeditereniaPicha: picture-alliance/AP/Turkish Energy Ministry

Maas ameongeza kuwa mvutano huo sio tu unayaweka mashakani mahusiano baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki, lakini utaharibu pande zote na kila mmoja anayehusika. Ugiriki inasema eneo ambalo meli ya Uturuki inaendesha operesheni zake inaingiliana na eneo lake na hivyo kuitaka Uturuki kuiondoa meli yake. Badala yake Uturuki ilijibu kwa kutuma taarifa za upanuzi wa shughuli za meli yake hadi Agosti 27 zinazojulikana kama Navtex na kuilazimu Ugiriki kutangaza luteka za kijeshi kwa muda wa siku tatu.

Pichani ni meli za Ugiriki zikisindikzwa na zile za UfaransaPicha: picture-alliance/AP Photo/Greek Defence Ministry/

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameonya kwamba "kuanzia sasa Ugiriki ndio inawajibika kwa lolote baya litakaloendelea katika ukanda huo", akiongeza kuwa mazoezi ya kijeshi yanahatarisha usalama wa pwani na meli zote katika kanda hiyo.

"Uturuki haitorudi nyuma kuondoa shughuli za meli ya Oruc Reic au meli za kivita zilizoambatana nayo. Badala yake itachukua hatua zaidi katika njia iliyo na nia ya kulinda haki zake katika ukanda huo. Anayehitaji kufikiria juu ya athari zitakazotokea baadae ni yule atakayekabiliana nasi kwenye eneo ambalo tumetangaza Navtex," alisema Maas.

Soma zaidi:Macron na Merkel wataka mzozo Belarus kutatuliwa

Mvutano huo unaozidi kuongezeka umeibua wasiwasi wa migogoro inayoweza kutokea baina ya wapinzani wawili wa kikanda, ambao wamewahi kufikia ukingoni mwa vita kwa mara tatu tangu katikati ya mwa miaka 1970, ikiwemo mara moja juu ya haki katika Bahari ya Aegean. Ziara ya Maas inafanyika pia kuelekea mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, utakaofanyika baadae wiki hii mjini Berlin.