1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heiko Maas na Makubaliano ya Mradi wa Nuklea wa Iran

Oumilkheir Hamidou
11 Juni 2019

Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani nchini Iran, vitisho vya Marekani vya kutaka kuitoza ushuru Mexico na maandamano ya umati wa raia wa Hong Kong ni miongoni mwa mada magazetini.

Bundesaußenminister Heiko Maas in Teheran
Picha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Tunaanzia Mashariki ya kati na hasa katika ghuba la Uajemi ambako waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas alifika ziarani  kwa lengo la kujaribu kuyaokoa makubaliano ya kimataifa ya mradi wa nuklea wa Iran baada ya Marekani kubatilisha makubaliano hayo. "Ni juhudi zinazostahiki sifa hata kama hazijaleta tija" linaandika gazeti la "Nordwest-Zeitung": "Binafsi  Heiko Maas hakuwa akiamini kama maendeleo yangepatikana. Hata hivyo ameifunga safari kwa lengo la kujaribu kuokoa kitakachoweza kuokoleka. Kilichojitokeza ni kwamba mbali na dhamiri njema za kujaribu kuupatia ufumbuzi mzozo wa nuklea, matokeo ya ziara hiyo ni haba.

Na hakuna kitakachobadilika mnamo muda wa hivi karibuni. Ufunguo wa mabadiliko unakutikana ama Washington au Teheran. Kwa wakati wote ambao Donald Trump atasalia kuwa rais wa Marekani hakuna kitakachobadilika. Kama Iran itaregeza kamba? Hadi sasa hakuna ishara. Kwa hivyo Ulaya kwa bahati mbaya haitokuwa na njia nyengine isipokuwa kukodowa macho.

Mvutano wa Marekani na Mexico haujamalizika

Mvutano kati ya Marekani na Mexico kuhusu mikururo ya wahamiaji wa Latin America unaonyesha kupatiwa ufumbuzi. Hata hivyo gazeti la "Badische-Neuste Nachrichten" linaonya kwa kuandika: "Donald Trump hajauzika bado mzozo wa ushuru pamoja na Mexico. Ameuweka kando tu. Inawezekana sana tena akaufukua wakati wowote ule. Hakuna anaeweza kuashiria kama atautumia miezi au wiki chache kutoka sasa kama mkakati wa kukandamiza au wa kutoa masharti ziada.

Taiwan yakodolea macho kinachotokea Hong Kong

Wakaazi milioni moja wa Hong Kong wameandamana mwishoni mwa wiki iliyopita kupinga mswaada wa sheria unaoruhusu wahalifu kuhamishiwa China bara ili kuhukumiwa. Chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya China bara na Uingereza, koloni hilo la zamani la Uingereza, Hong Kong litaendelea kujivunia mfumo wake wenyewe wa kijamii, kisheria na kisiasa kwa miaka 50 tangu makubaliano hayo yalipotiwa saini mwaka 1997. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika jinsi Taiwan, ambayo pia China bara inadai ni milki yake, inavyoyaangalia maandamano ya Hong Kong: "Taiwan ikitaka kujua, kinachowasiibu watu wanaoishi chini ya uongozi wa Peking, inaangalia kinachotokea Hong Kong.

"Nchi moja mifumo miwili ndio kauli mbiu tangu China bara ilipokabidhiwa kanuni maalum mwaka 1997 kuhusu koloni hilo la zamani la Uingereza. Sasa wenye madaraka mjini Peking wanataka kutunisha misuli. Kwasababu kinyume na wakaazi wa China bara, wale wa Hong Kong wanajivunia uhuru na wanatambua watakosa nini pindi wakipokonywa uhuru huo.

 

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW