1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

Helikopta iliyowabeba watu 22 yatoweka Urusi

Angela Mdungu
31 Agosti 2024

Helikopta iliyobeba watu 22 wengi wao watalii imepotea katika rasi ya Kamchatka nchini Urusi. Vladimir Solodov gavana wa jimbo hilo amesema helikopta hiyo chapa Mi-8 ilipoteza mawasiliano saa kumi na dakika tano.

Helikopta ya Urusi iliyowabeba watu 22 imetoweka Kamchakta
Timu ya waokoaji ilipokuwa ikiitafuta Helikopta chapa Mi-8 Julai 2021. Helikopta kama hiyo imetoweka Agosti 31, 2024 Picha: Russian Emergencies Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Timu za uokoaji zinaendelea na juhudi za kukitafuta chombo hicho.Chanzo kimoja kutoka huduma za dharura kililiambia shirika la Habari la Urusi la TASS kuwa, helikopta hiyo ilitoweka katika rada muda mfupi baada ya kupaa na wahudumu wake hawakuripoti tatizo lolote katika chombo hicho.

Ajali zinazohusisha ndege na helikopta zimekuwa za mara kwa mara katika eneo hilo la mashariki ya mbali nchini humo lenye watu wachache na linalokabiliwa na hali mbaya ya hewa mara kwa mara.

Wakati huohuo, kituo huru cha habari cha Urusi cha Mediazona kimesema leo kinakadiria kuwa zaidi ya wanajeshi 66,000 wa Urusi wameuwawa kwenye vita vinavyoendelea kati ya taifa hilo na Ukraine.

Soma zaidi: Urusi, Ukraine zatupiana lawama kuanguka ndege ya wafungwa

Kituo hicho kimekuwa kikiweka kumbukumbu ya orodha ya vifo vinavyoripotiwa vya wanajeshi wa Urusi kwa kushirikiana na Shirika la habari la BBC. Awali mwezi Aprili, Mediazona iliripoti kuwa ilipata zaidi ya majina 50,000 ya Warusi waliouwawa vitani. Kituo hicho kimesema kuwa kufikia Agosti 30, majina yanayofahamika ya wanajeshi wa Urusi waliouwawa katika vita hivyo ni 66,471.

Pamoja na ripoti hiyo, kituo hicho kimesisitiza kuwa, majina hayo si idadi kamili kwani vifo vya wanajeshi walio wengi havitangazwi hadharani. Mwandishi wa habari wa Mediazona Anastasia Alekseyeva ameongeza kuwa, idadi hiyo ya sasa ya vifo haihusiani na idadi ya wanajeshi wa Urusi waliouwawa katika uvamizi uliofanywa na Ukraine katika mji wa Kursk au mapambano yaliyoiwezesha Urusi kusonga mbele katika upande wa mashariki.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW