HELIKOPTA ZA MAREKANI ZAGONGÁNA
16 Novemba 2003BAGHDAD: Helikopta mbili za Kimarekani aina ya "Black Hawk" zimegongana angani katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq.Wanajeshi 17 wamefariki 5 wamejeruhiwa na mmoja anakosekana.Kwa mujibu wa mashahidi ikiwa ni pamoja na afisa mmoja wa Kimarekani,kombora liliipiga helikopta moja,na hiyo ikaiangukia helikopta ya pili.Wakuu wa kijeshi lakini wamesema hawatokisia sababu ya helikopta hizo kugongana bali watangojea mpaka utakapofanywa uchunguzi.Hapo awali mkuu wa kiraia wa Kimarekani nchini Iraq Paul Bremer na Baraza Tawala la Wairaqi lililoteuliwa na Marekani,walikubaliana kuunda serikali ya mpito itakayoongozwa na Wairaqi wenyewe.Kwa mujibu wa kiongozi wa Baraza Tawala bwana Jalal Talabani serikali ya mpito itashika madaraka mwezi Juni mwaka ujao.Serikali hiyo itachaguliwa na baraza la wajumbe kutoka mikoa 18 ya Iraq.Baadae kutaundwa katiba na uchaguzi mkuu utafanywa mwishowe wa mwaka 2005.Kwa wakati huo huo rais George W.Bush wa Marekani amesema vikosi vitabakia nchini mpaka hali ya utulivu itakaporejea Iraq.Lakini Talabani amesema ikiwa vikosi vya Kimarekani havitahitajiwa baada ya mwaka ujao,basi vikosi hivyo vitaombwa viondoke.
