1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heri ya mwaka mpya! Ulimwengu wakaribisha 2025

1 Januari 2025

Miji kote ulimwenguni imeukaribisha Mwaka Mpya kwa sherehe za kukata na shoka zilizoangazia tamaduni mbalimbali. New Zealand na mashariki mwa Australia zilikuwa nchi za kwanza kuukaribisha mwaka wa 2025.

Fataki ziliimulika anga juu ya sanamu la Quadriga katika Lango la Brandenburg wakati wa sherehe za Mwaka Mpya muda mfupi baada ya saa sita usiku, Berlin, Ujerumani
Berlin yaukaribisha mwaka mpya wa 2025Picha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

Auckland ulikuwa wa kwanza mkubwa kusherehekea, huku maelfu ya watu wakimiminika katikati ya mji au kupanda kwenye vilele vya milima ya volcano ili kuwa na nafasi nzuri ya kuziona fataki. Nchi za Bahari ya Pasifiki Kusini zilikuwa za kwanza kuukaribisha mwaka mpya.

Migogoro ilinyamazisha sherehe za kuanza kwa 2025 katika maeneo kama vile Mashariki ya Kari, Sudan na Ukraine.

Kulikuwa na matamasha ya muziki na kwa wengine walikesha makanisani kabla ya maonesho ya kufyatua fataki mara tu ilipotimia saa sita kamili za usiku.

Umoja wa Falme za Kiarabu uliukaribisha mwaka mpya kwa fataki kwenye jengo refu kabisa duniani la Burj Khalifa DubaiPicha: Amr Alfiky/REUTERS

Hapa Ulaya makumi ya maelfu ya watu walikusanyika mbele ya Lango la Brandenburg mjini Berlin, Ujerumani, huku fataki zikiimulika anga kwa rangi za kupendeza. Huko Paris, onyesho kubwa la fataki kwenye mtaa wa Champs-Élysées lilivutia takriban watu milioni moja. Umoja wa Falme za Kiarabu uliukaribisha mwaka mpya kwa fataki kutokea kwenye jengo refu kabisa duniani la Burj Khalifa Dubai.

London iliukaribisha mwaka mpya kwa maonesho makubwa ya fataki kwenye Mto Thames. Huku kimbunga kikisababisha hali mbaya ya hewa katika maeneo mengine ya Uingereza, hata hivyo, sherehe mjini Edinburgh, Scotland, zilifutwa.

Nchini Korea Kusini, sherehe zilipunguzwa au kufutwa kutokana na kipindi cha maombolezo ya kitaifa kufuatia ajali ya ndege ya shirika la Jeju Air iliyoua watu 179.

Miji nchini Syria iliadhimisha Mkesha wa Mwaka Mpya kwa sherehe kubwa chini ya ulinzi mkali, wiki chache tu baada ya kuangushwa mtawala wa zamani Bashar al-Assad.

Wasyria walisherehekea Mwaka Mpya kote nchini humo chini ya ulinzi mkaliPicha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Rais wa Xi Jinping na rais wa Urusi Vladmir Putin waliukaribisha mwaka kwa kutumiana salamu kuashiria kuongezeka kwa ufariki kati ya viongozi hao wawili wanaokabiliwa na mivutano na nchi za magharibi.

Makumi kwa maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono Umoja wa Ulaya waliukaribisha mwaka wa 2025 kwa kukusanyika nje ya bunge la Georgia.

Rais wa zamani Salome Zurabishvili - ambaye anazozana na chama tawala cha Georgian Dream kuhusu uchaguzi wenye utata wa Oktoba na yeye mwenyewe kuondolewa madarakani - alijiunga na waandamanaji.

Muhula wa Zurabishvili ulimalizika Jumapili wakati Mikheil Kavelashvili wa chama tawala alipoapishwa kuwa mkuu wa nchi, baada ya kuwa mgombea pekee katika mchakato wa uteuzi uliosusiwa na upinzani uliofanywa na jopo maalum la uchaguzi, badala ya kura ya umma.

Katika ujumbe wa Mwaka Mpya, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema 2025 inaleta "matumaini mapya na dhamira kuchapa kazi."

"Kutoka kwa nguvu ya kiuchumi hadi usalama, ulinzi na ushirikiano wa kimataifa, timu yangu na mimi tuko tayari kufanya kazi kwa ajili ya Ulaya yenye nguvu zaidi, ndani na nje ya bara hilo," aliahidi kwenye mitandao wa kijamii.

Afp, dpa, ap, reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW