1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hertha Berlin inawinda tikiti ya Champions League

7 Machi 2016

Hertha Berlin iko kwenye mkondo wa kurejea katika kandanda la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2000 licha ya kichapo cha kushangaza cha mabao mawili kwa sifuri na Hamburg

Fussball Bundesliga 26. Spieltag 06.03. 2016 Hamburger SV vs. Hertha BSC
Picha: Getty Images/AFP/S. Franklin

Hertha inayoongozwa na kocha Pal DARDAI iko nyuma ya nambari mbili Borussia Dortumund na pengo la pointi 16 na nyuma ya viongozi wa ligi Bayern Munich na tofauti ya pointi 21, lakini inashikilia nafasi ya tatu pointi moja mbele ya Schalke, ambayo itaialika mjini Berlin Ijumaa ijayo.

Awali, nambari tano kwenye ligi Mainz iliyocheza na wachezaji kumi ilishindwa ilitoka sare ya kutofungana bao na Darmstadt lakini bado pia imo katika kundi linalowinda kandanda la Champions League pamoja na Schalke, Wolfsburg na Borussia Moenchengladbach. Kocha wa Mainz Martin Schmidt aliuzunguzia mchuano huo "Mchezo ulikuwa na vipindi viwili. Kipindi cha wachezaji 11 na kingine cha wachezaji kumi. Katika sehemu tuliyokuwa 11 hatukucheza vizuri. Na kisha tulipokuwa kumi, nadhani tulijitahidi sana, tukapambana na kuudhibiti mpira na ndio maana haungeweza kuona kuwa tulikuwa na upungufu wa mchezaji mmoja. Na kwa hivyo naipongeza sana timu yangu".

Siku ya Jumamosi, viongozi Bayern Munich walisalia kileleni na pengo la pointi tano mbele ya mahasimu wao wa karibu katika Bundesliga Dortmund baada ya kutoka sare tasa katika mpambano wao mkali wa der Klassiker.

Picha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

Licha ya ukosefu wa mabao, kipute hicho kilitimiza matarajio ya wengi kutokana na msisimko ulioshuhudiwa uwanjani kutoka kwa mahasimu hao wawili katika uga wa Dortmund wa Signal Iduna Park ambao ulifurika hadi pomoni. Thomas Muller ni mshambualiji wa Bayern "Ulikuwa mchuano mkali wa sare ya bila bila. Hasa katika kipindi cha kwanza kila timu ilikuwa na nafasi lakini nimeona katika kipindi cha pili tulituluza mambo na kudhibiti mchezo. Hivyo ilikuwa sare ya kusisimua ya bila bila. Nadhani ilichosha sana na tumeridhika".

Erik Durm alihakikisha kuwa ngome ya Dortmund ilikuwa imara dhidi ya mashambulizi ya Bayern "matokeo haya ni kama kichapo, lakini Sijui. Kilikuwa kitu cha kushangaza kwamba tulitoka sare mwishowe. Lakini tulitaka zaidi ya hilo. Tulitaka kushinda, na kupunguza pengo kati yao na sisi. Lakini nadhani sote tunaweza kuridhika na pointi. Lakini bila shaka tulitaka kushinda".

Awali, Bayer Leverkusen ilitoka nyuma mabao 3-0 na kuepuka kichapo cha nne mfululizo kwenye ligi kwa kulazimisha sare ya mabao matatu kwa matatu na Augsburg. Wolfsburg ilipasha misuli moto kabla ya mchuano wake wa Champions League dhidi ya Gent hapo kesho, kwa kuilaza Moechengöadbach mbili moja. Ushindi huo uliosogeza Wolfsburg hadi nafasi ya saba. Sare ya moja kwa moja ya Eintracht Frankfurt nyumbani dhidi ya Ingolstadt iligeuka kuwa mchuano wa mwisho kwa kocha Armin Veh wakati akipigiwa kalamu jana baada ya klabu hiyo kutumbukia katika nafasi ya kushushwa ngazi.

Werder Bremen iliendelea kujiondoa kabisa katika eneo la mkia, baada ya kuwazaba washika mkia Hanover nne moja. Stuttgart waliwabwaga nambari mbili kutoka nyuma Hoffenheim tano moja wakati Schalke ikisonga hadi nafasi ya nne kufuatia ushindi wa tatu moja dhidi ya Cologne.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman