1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Kifo cha Raisi: Waombolezaji watoa heshima za mwisho

Angela Mdungu
21 Mei 2024

Maelfu ya raia wa Iran, wanatoa heshima zao mwisho kwa aliyekuwa kiongozi wa taifa lao Ebrahim Raisi, na maafisa wengine waliofariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili.

Ebrahim Raisi na maafisa wengine saba walikufa kwa ajali ya helikopta Mei 19,2024
Waombolezaji kando ya gari lililobeba jeneza la Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine saba mjini TabrizPicha: Fatemeh Bahrami/Anadolu/picture alliance

Raia hao mamia kwa maelfu waliobeba bendera za taifa hilo na picha za Ebrahim Raisi wameshuhudiwa katika uwanja wa Central square mjini Tabriz wakitembea kando ya gari lililobeba majeneza ya Raisi na maafisa wengine saba.

Mji huo ndiko alikokuwa akielekea kiongozi huyo na ujumbe wake wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipopata ajali Jumapili. Mwili wa Raisi utasafirishwa kwa ndege kuelekea mji wa Qom na baadaye leo kabla ya kuelekea mji mkuu, Tehran, jioni.

Soma zaidi:Mokhber: Hakuna kitakachoharibika Iran

Maandamano makubwa ya kutoa heshima za mwisho na gwaride vitafanyika katika mji huo mkuu Jumatano asubuhi kabla ya Kiongozi Mkuu wa Kidini na Kisiasa wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei kuongoza ibada ya kumuaga.

Maziko ya Raisi kufanyika Alhamisi

Mwili wa Raisi unatarajiwa kusafirishwa baada ya hapo kuelekea nyumbani kwake katika mji wa Mashhad anakotarajiwa kuzikwa Alhamisi katika msikiti wa Imam Reza.

Raisi Ebrahim Raisi, waziri wake wa mambo ya kigeni Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine, walipata ajali hiyo walipokuwa wakitokea katika uzinduzi wa mradi wa pamoja na Azerbaijan wa bwawa la kufua umeme katika mto Aras. Mto huo ni sehemu ya mpaka wa Azerbaijan na Iran na uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Rais Ilham Aliyev.

Raia wa Iran wakiomboleza kifo cha Rais Ebrahim Raisi Picha: Sha Dati/Xinhua/IMAGO

Soma zaidi: Iran kufanya uchaguzi mkuu wa rais mnamo Juni 28

Helikopta iliyokuwa imembeba Raisi ilipoteza mawasiliano ilipokuwa ikirejea Tabriz baada ya shughuli hiyo. Televisheni ya taifa ya Iran ilitangaza kifo cha kiongozi huyo na abiria wote waliokuwa kwenye helikopta hiyo Jumatatu baada ya saa kadhaa za operesheni ya uokoaji.  Tayari serikali ya Iran imeagiza uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

Soma zaidi: Rais wa Iran amefariki katika ajali ya helikopta

Kutokana na msiba huo, Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, alitangaza siku tano za maombolezo na ameshamthibitisha aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais Mohammad Mokhber, kuwa kaimu raisi. Kulingana na shirika la habari la Iran, uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaopaswa kufanyika ndani ya siku hamsini baada ya kifo cha Raisi, unatarajiwa kufanyikaJuni 28.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW