Heynckes atunukiwa tuzo ya kocha bora Ujerumani
3 Aprili 2015Kocha huyo wa zamani wa Bayern Munich Jupp Heynckes ndiye kocha wa tano kutambuliwa kwa “kazi yake maishani ya ukufunzi”.
Heynckes mwenye umri wa miaka 69 alianza taaluma yake ya ukufunzi mwaka wa 1979 katika klabu ya Borussia Moenchengladbach.
Baada ya kupigiwa kura ya kuwa Kocha Bora wa FIFA katika Mwaka wa 2013, Heynckes alipokea tuzo hiyo mjini Bonn, katika hafla ya 61 ya mafunzo ya makocha wa kandanda, ambayo huwatambua makocha chipukizi wa Ujerumani wanaokamilisha mpango mkali na wa hali ya juu wa DFB kuhusu ukufunzi.
Heynckes alistaafu ukufunzi baada ya kushinda mataji matatu mwaka wa 2013, akiwa na Bayern. Tuzo hiyo kuu ya Kocha Bora Ujerumani imewahi kupewa tu watu wengine wanne: Dettmar Cramer, Udo Lattek, Gero Bisanz na Otto Rehhagel.
Wakati huo huo, kocha wa timu ya wanawake ya Ujerumani kwa wachezaji wa chini ya umri wa miaka 20 Maren Meinert alichukua Tuzo ya Kocha wa Bora wa Ujerumani wa Mwaka wa 2014 kutokana na huduma zake za kukuza vipaji.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu